1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjomba wa Kim Jong Un anyongwa!

13 Desemba 2013

Korea ya Kaskazini imesema Ijumaa(13.12.2013) imemnyonga mjomba wa kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-Un na mtu mwenye ushawishi mkubwa wa utawala wa nchi hiyo, Jang Song-Thaek, kwa hatia za usaliti wa zama zote.

https://p.dw.com/p/1AYmt
Jang Sung-taek akiwa katika mahakama ya kijeshi alikohukumiwa kifo. (13.12.2013).
Jang Sung-taek akiwa katika mahakama ya kijeshi alikohukumiwa kifo. (13.12.2013).Picha: Reuters

Katika muadhara wa kushutusha Jang, ambaye alikuwa akionekana kama ni kaimu wa kisiasa wa Kim na mtu anayeshika nafasi ya pili katika uongozi wa nchi hiyo, alinyongwa hapo jana mara tu baada ya kusikilizwa kwa kesi yake na mahakama maalum ya kijeshi.

Shirika la habari la serikali ya Korea ya Kaskazini, KNCA, limesema katika taarifa iliyomshutumu vikali Jang, kwamba alitiwa hatiani kwa uhalifu wa kificho wa kuipinduwa serikali kwa kutumia njia zote za chokochoko na hizaya kwa tamaa ya wazimu wa kunyakuwa madaraka ya chama na taifa.

Ripoti hiyo imemuelezea Jang kuwa ni mlevi na mla rushwa ambaye ametanuwa makucha yake katika kila ya fani ya masuala ya taifa. Katika kukiri hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo ambalo ni jambo la nadra pia imemlaumu kwa kushindwa kuwasaidia watu wanaokabiliwa na njaa nchini humo na umaskini wa taifa hilo.

Mwanahizaya

Ripoti hiyo imelaani Jang kuwa ni kiumbe mwana hizaya mbaya kuliko hata mbwa ambaye alijaribu kukwamisha mchakato wa Kim-Jong Un kurithi nafasi ya baba yake na kumuandama kwa jaribio la mapinduzi.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akiwa na mjomba wake Jang Song-Thaek.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akiwa na mjomba wake Jang Song-Thaek.Picha: Reuters/Kyodo/File


Jang mwenye umri wa miaka 67 alikuwa na dhima muhimu katika kuimarisha uongozi wa Kim ambaye alikuwa hana uzoefu wakati aliporithi nafasi ya baba yake Kim Jon-Il hapo mwaka 2011, lakini wachambuzi wanasema madaraka na ushawishi wake umekuwa ukizidi kuchukiwa nchini humo.

Vyombo vya habari vya taifa vimemuonyeha Jang aliyepwaya akiwa na pingu mkononi akiondolewa kwenye mahakama hiyo ya kijeshi akisindikizwa na maafisa wawili.

Marekani na Korea Kusini zafadhaishwa

Naibu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Marie Harf, amesema kunyongwa huko kwa Jang ni mfano mwengine wa jinsi utawala wa Korea Kaskazini ulivyo katili na ameongeza kusema kwamba serikali ya Marekani inafuatilia kwa makini matukio hayo.

Rais wa Korea ya Kusini, Park Guen -Hye, amemshutumu Kim Jong-Un kwa kutumia vitisho kuimarisha uongozi wake. Waziri wa masuala ya muungano ya Korea ya Kusini Kim Eui Do leo ameelezea wasi wasi wake mkubwa wa nchji hiyo juu ya hali hiyo.

Rais wa Korea Kusini Park Geun Hye.
Rais wa Korea Kusini Park Geun Hye.Picha: AHN YOUNG-JOON/AFP/Getty Images

Korea ya Kaskazini ilithibitisha mapema wiki hii kwamba Jang ambaye amemuowa shangazi wa Jong-Un, amevuliwa nyadhifa zake zote na kumwita kuwa ni mtu mwenye kutumia madawa ya kulevya na mwenye kupenda wanawake ambaye amefanya ubadhirifu wa mamiloni ya fedha za taifa katika vilabu vya kamari vya kigeni.

Wakati wa kesi yake, imeripotiwa kwamba Jang alikiri kwamba alifanya jaribio la kuiangusha serikali kwa kuwashawishi washirika wake jeshini.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Khelef