1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Zinjibar wakombolewa kutoka kwa waasi Yemen

Mjahida 10 Agosti 2015

Maafisa wa kijeshi Yemen wamesema wapiganaji wanaoiunga mkono serikali, wameudhibiti mji wa Zinjibar nchi humo. Hii ni baada ya siku tatu za mapigano, kati yao na waasi wa kishia wa Houthi pamoja na washirika wake.

https://p.dw.com/p/1GCeu
Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali ya Yemen
Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali ya YemenPicha: Getty Images/AFP/S. Al-Obeidi

Mji wa Zinjibar, katika mkoa wa Abyan ulikombolewa siku moja baada ya shambulizi la angani kutoka kwa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, kuwashambulia kimakosa wapiganani hao walipokuwa wakisafiri kuelekea mji wa Zinjibar na kusababisha mauaji ya watu 20.

Muungano huo wa Saudi Arabia unaoungwa mkono na Marekani ulianza mashambulizi yake mwezi Machi dhidi ya waasi wa kishia wa Houthi, na washirika wake waliotiifu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh, wanaoudhibiti mji mkuu Sanaa na maeneo mengine mengi Kaskazini mwa Yemen.

Waasi hao wanapigana dhidi ya watu wa kusini wanaotaka kujitenga, wanamgambo wa ndani na wa kikabila, wanamgambo wa kisuni, na watu tiifu kwa rais aliyeuhamishoni Abed Rabbo Mansour Hadi.

Wakaazi wa kusini mwa Yemen wanaoisaidia serikali kupambana na waasi wa Houthi
Wakaazi wa kusini mwa Yemen wanaoisaidia serikali kupambana na waasi wa HouthiPicha: Reuters/Str

Maafisa wa kijeshi wamesema katika mapigano ya Zinjibar, kulishuhudiwa vifaru vya kisasa vya kijeshi na magari ya kivita, yaliowapa nguvu wapiganaji waliotiifu kwa serikali. Vifaa hivyo vinasemekana kutolewa na serikali ya Saudi Arabia pamoja na nchi ya falme za kiarabu. Hata hivyo nchi zote mbili bado hazijakubali kutuma wanajeshi wake katika eneo hilo la vita.

Lakini awali Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) ulisema, wanajeshi wake watatu waliuwawa wakati waliposhiriki kampeni inayoongozwa na Saudi Arabia. Taarifa hiyo iliyoripotiwa na chombo cha habari cha WAM, haikueleza zaidi vipi au wapi wanajeshi hao walivyouwawa. Vifo vya hivi karibuni vinafikisha wanajeshi wa Imarati waliouwawa kufikia watano, katika mapigano dhidi ya waasi wa Houthi yaliyoanza mwezi Machi.

Washirika wa Houthi wateka nyara watu kadhaa

Kwa upande wao maafisa nchini yemen wamesema washauri wa kijeshi kutoka serikali za nchi ya falme za kiarabu, Misri, na Jordan wanatoa mafunzo kwa wapiganaji kadhaa kwenye kambi ya kijeshi karibu na mji wa Aden. Maafisa wote waliozungumza hawakutaka kujulikana kwa sababu hawakuwa na ruhusa ya kuzungumza na waandishi habari.

Gari la waasi wa Houthi lililoteketezwa moto mkoani Lahej
Gari la waasi wa Houthi lililoteketezwa moto mkoani LahejPicha: Reuters/Str

Huku hayo yakiarifiwa hapo jana wapiganaji wanaoaminiwa kuwa na mafungamano na waasi wa Houthi waliwateka nyara watu kumi, ambao ni wanachama wa Islamist Al-Islah. Akiwemo waziri wa zamani wa serikali na mwanamke mmoja. Hii ni kulingana na jamaa za watu waliotekwa.

Haya yakijiri, mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu amefanya ziara ya siku tatu katika mji wa kale wa Sanaa uliowekwa kuwa eneo la turathi za zamani na shirika la umoja mataifa la elimu sayansi na tamaduni UNESCO.

Peter Maurer aliwasili mjini sanaa siku ya Jumamosi kuangalia hali halisi ya mji huo, na hasara iliopatikana kutokana na vita. Umoja wa Mataifa umesema watu takriban 4,000 wameuwawa tangu mapigano kuanza mwenzi Machi, huku asilimia 80 ya idadi ya watu milioni 21 nchini Yemen wakihitaji msaada wa kiutu na kulindwa. Shirika la Msalaba Mwekundu limesema, watu milioni 1.3 wameachwa bila ya makaazi.

Muandishi: Amina Abubakar AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef