Mji wa Sanaa washambuliwa kwa makombora
31 Machi 2020Muungano huo wa kijeshi umesema operesheni hiyo ya kijeshi iliyalenga maeneo ya kuunda na kuhifadhi makombora ya masafa marefu pamoja na ndege zisizo na rubani kwenye viunga vyote vilivyo chini ya udbiti wa waasi wa Houthi.
Walioshuhudia wamesema vituo kadhaa vilivyo muhimu ikiwemo Ikulu ya rais, majengo ya shule moja na kambi ya kijeshi karibu na uwanja wa ndege wa mjini Sanaa vilishambuliwa na sauti kubwa ya miripuko ilisikika kote mjini humo.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umesema mashambulizi hayo yalinuwia kuharibu kabisa miundombinu yote ya kijeshi inayotishia maisha ya raia kwenye maeneo yanayoshikiliwa na waasi.
Mashambulizi ya kulipa kisasi
Televisheni inayomilikiwa na waasi wa Houthi Al-Masirah imesema mpiganaji wake mmoja ameuwawa na wengine wawili kujeruhiwa wakati makombora yalipokilenga chuo moja ya mafunzo ya kijeshi.
Sehemu ya makombora yaliyokipiga chuo hicho ilianguka kwenye zizi la farasi na kuwauwa farasi 70 na kujeruhi wengine zaidi ya 30.
Mashambulizi hayo yamefanyika baada ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Saudi Arabia kuyakabili na kuyaharibu makombora yaliyorushwa na wahouthi na kuilenga miji ya Riyadh na Jizan siku ya Jumamosi.
Tukio hilo liliwauwa watu wawili mjini Riyadh na lilikuwa shambulizi kubwa la kwanza kutekelezwa na waasi wa Houthi dhidi ya Saudi Arabia tangu waasi hao walipoahidi Septemba iliyopita kusitisha mapigano baada ya kuilenga kwa makombora miundombinu ya mafuta nchini Saudia.
Mashambulizi kwenye mji mkuu Sanaa yamekuwa jambo la nadra tangu wakati huo baada ya Saudi Arabia kuanzisha mazungumzo yasiyo ya moja moja na vuguvugu la wahouthi linalodhibiti mji huo na sehemu kubwa ya kaskazini ya Yemen.
Wito wa kusitishwa mapigano wapuuzwa
Makabiliano hayo yanatokea licha ya pande zote hasimu katika vita nchini Yemen kuunga mkono wito wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa kusitisha mapigano ili kushughulikia kadhia ya virusi vya Corona.
Saudi Arabia, Serikali ya Yemen na waasi wa Houthi walilikaribisha pendekezo la Guterres la kukomesha mashambulzii na kuisadia Yemen kuepuka kishindo cha janga la Corona.
Yemen bado haijarikodi kisa chochote cha ugonjwa wa COVID-19 lakini kuna wasiwasi mkubwa kuwa mfumo wa afya uliozorota nchini humo utashindwa kukabiliana na maradhi hayo pindi yatakapolikumba taifa hilo.
Nchi hiyo tayari inakabiliwa na kile Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.