1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Dar es Salaam wapata mkuu mpya, Aboubakar Kunenge

Hawa Bihoga Dw Dar es salaam3 Agosti 2020

Aliekuwa mkuu wa mkoa wa dar es salaam Paul Makonda amekabidhi ofisi kwa mkuu mpya wa mkoa ambae aliteuliwa na Rais Magufuli mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/3gLvX
Tansania Daressalam Paul Makonda
Picha: DW/S. Khamis

Katika makabidhiano hayo Makonda ambae aliachia ukuu wa mkoa baada ya kujitosa kwenye ulingo wa kisiasa amekiri kutokamilisha mambo kadhaa ikiwemo kuwapima wakaazi wajiji hilo tezi dume.

Mapema Jumatatu Makonda alifika katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kwa dhima moja tu ya kukabidhi ofisi hiyo alioihudumu kwa takriban miaka mitano.

Punde baada ya kukabidhi akielezea mafanikio na changamoto ambazo amekabiliana nazo, amesema, miongoni mwa mambo ambayo hakuyafanikisha ni pamoja na kampeni ya upimaji wa tezi dume kwa wakaazi wa mkoa huo, kutokana na wengi kusita kupima maradhi hayo.

Uongozi wa Makonda ulikuwa wa aina gani?

Katika kipindi cha uongozi wake Makonda anatajwa kuanzisha kampeni mbalimbali ambazo zilizua gumzo ikiwemo ile ya kuwataja washukiwa wanaouza dawa za kulevya hadharani pamoja na ile ya kuwapima wanaume walioshukiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, amesema alikabiliana na changamoto kadhaa huku zingine zilihatarisha hata uhai wake.

Mji wa Dar es Salaam. (Picha ya maktaba- 21.03.2018)
Mji wa Dar es Salaam. (Picha ya maktaba- 21.03.2018)Picha: DW/Eric Boniphace

Sehemu ya changamoto ambazo Makonda alikutana nazo kwa kiwango kikubwa ni pamoja na kukosolewa kwenye mitandao ya kijamii hatua ambayo anakiri ilileta changamoto kubwa katika uongozi wake, hivyo kumtaka mkuu huyo wa mkoa mpya kuhakikisha anatekeleza majukumu yake bila kuzingatia hoja alizozitaja potofu katika mitandao ya kijamii.

Mafanikio ya Makonda Dar

Makonda ambae amekaa mamlakani takriban miaka mitano anatajwa kufanikisha masuala kadhaa ikiwemo, kupunguza idadi ya ombaomba kwenye jiji, kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia kupitia kampeni yake ya wanawake waliotelekezwa na wenza wao baada ya kupewa ujauzito au kujifungua.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa mpya ambae pia alikuwa katibu tawala katika kipindi cha uongozi wa mwanansiasa huyo kijana Aboubakari Kunenge amesema kipindi chake cha uongozi kitaendelea kufanikisha yale ambayo mkuu huyo wa mkoa mstaafu hakuyafanikisha kutokana na sababu kadhaa.

Makonda amekuwa akikosolewa vikali hadharani kutokana na matamshi yake yaliotafsiriwa kukiuka haki za binadamu na hata kuwekewa vizuizi katika mataifa kadhaa ikiwemo Marekani. Alishika nafasi ya pili katika kura za maoni katika kuwania ubunge wa Kigamboni.