Mjerumani atekwa nyara nchini Afghanistan
17 Desemba 2007Polisi nchini Afghanistan leo wamethibitisha kwamba mjerumani mmoja mfanyakazi wa zamani wa shirika la kutoa misaada nchini Afghanistan ametekwa nyara pamoja na familia yake.
Duru za polisi zinasema watu wanne waliokuwa wamejihami na bunduki walilmazimisha seremala huyo wa kijerumani mwenye umri wa miaka 42 atoke nje ya motokaa yake katika mkoa wa Herat, magharibi mwa Afghanistan hapo jana usiku.
Gazeti la hapa Ujerumaji, Suddeutsche Zeitung, limemtaja mwanamume huyo kuwa Harald Kleber ambaye amekuwa akiishi nchini Afghanstan tangu mwaka wa 2003. Shirika la misaada la Green Helmets la Ujerumani, alilolifanyia kazi seremala huyo limesema mke wa bwana Kleber pamoja na watoto wake pia wametekwa nyara.
Wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani inachunguza taarifa hizo.
Miezi mitano iliyopita mhandishi wa kijerumani, Rudolf Blechschmidt, alitekwa nyara lakini akaachiliwa baada ya miezi mitatu. Mjerumani mwingine aliyetekwa nyara pamoja naye alikufa wakati alipokuwa akizuiliwa na watekaji nyara.