Mjerumani atekwa nyara kaskazini mwa Somalia
12 Februari 2008Matangazo
Raia mmoja wa Ujerumani anayefanyakazi na shirika la kutoa misaada kaskazini mwa Somalia, ametekwa nyara leo. Shirika la misaada la kijerumani la Deutsche Welthungerhilfe, limethibitisha utekaji nyara huo.
Kwa mujibu wa wakaazi wa eneo la Erigabo, lililo takriban kilomita 900 kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu, dereva wa mfanyakazi huyo amejeruhiwa wakati wa uvamizi uliofanywa na watu waliokuwa wamejihami na silaha.
Wizara ya mashauri ya kigeni ya Ujerumani mjini Berlin inachunguza habari za kutekwa nyara kwa mjerumani huyo.
Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana, wafanyakazi wawili wa kigeni wa shirika la misaada la madaktari wasio na mipaka, walitekwa nyara kaskazini mwa Somalia, lakini wakaachiwa baada ya juma moja.