1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa televisheni wachambuliwa magazetini

10 Septemba 2013

Nani ameibuka na ushindi katika mjadala pekee wa televisheni kabla ya uchaguzi mkuu september 22 ijayo?

https://p.dw.com/p/19a4Y
Picha: picture-alliance/dpa

Homa ya uchaguzi mkuu inazidi kupanda nchini Ujerumani na mjadala pekee wa televisheni kati ya mtetezi na mgombea kiti cha kansela, Angela Merkel na Peer Steinbrück umewazinduwa wale ambao hadi jana usiku walikuwa bado hawajaamua nani wa kumpa kura zao. Mbali na hayo magazeti ya Ujerumani hii leo yamemulika pia kizungumkuti cha Syria na uamuzi wa rais Barak Obama kupata ridhaa ya bunge kabla ya kumtia adabu Bashar Al Asaad kwa kukiuka mstari mwekundu.

Tuanzie lakini hapa hapa Ujerumani ambako mamilioni ya watu walijionea mjadala pekee wa televisheni kati ya kansela Angela Merkel wa chama cha CDU na mshindani wake Peer Steinbrück wa chama cha upinzani cha SPD kabla ya uchaguzi mkuu September 22 ijayo. Maoni yanatofautiana kati ya taasisi za utafiti wa maoni ya umma. Hata hivyo gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika:

Peer Steinbrück hajakubali kushindwa:Ametoa maelezo ya kina na mzaha juu yake, huku akionekana kujiamini kabisa. Angela Merkel amejitokeza kama kawaida yake akiwa na msimamo thabiti kuelekea ulaya, na mkakamavu. Mjadala wa televisheni kati ya mgombea kiti cha kansela kutoka chama cha SPD na kansela Merkel haujazusha maajabu ya kina. Kwa jumla mtu anaweza kusema mgombea alikuwa mkali zaidi kuliko wengi walivyokuwa wakitegemea naye mkuu wa serikali akionekana kujiamini kama ilivyotarajiwa.

Steinbrück aridhisha

Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linahisi Steinbrück ndiye aliyekata kiu cha wale waliokuwa wakifuatilizia mjadala huo. Gazeti linaendelea kuandika:

Steinbrück amefanya vizuri sana-na baadhi ya wakati alikuwa mcheshi kama alivyokuwa zamani,kabla ya kuteuliwa na SPD kuwa mgombea kiti cha kansela.Alijadiliana na kansela Angela Merkel bila ya hofu,kwa kujiamini na kuheshimiana.Hilo limemsaidia kurejesha hadhi yake iliyoanza kuchujuka.Lakini ndo kusema itamsaidia pia kunyakua kiti cha kansela?Hasha.Ushawishi wa mjadala wa televisheni una kikomo katika uchaguzi-kama wasemavyo wachunguzi wa maoni ya umma.Kuna waliokuwa wakiuangalia mjadala huu kama fursa ya mwisho kwa Steinbrück.Ameitumia ipasavyo.Lakini kuanzia leo anarejea tena katika pirika pirika za kampeni ya uchaguzi.Na katika uwanja huo,msimamo ya mwanasiasa huyo wa chama cha SPD na ule wa Merkel inalingana yanapohusika masuala muhimu mfano mzozo wa Syria,au jinsi ya kuiokoa sarafu ya Euro.

Obama aregeza kamba

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na kizungumkuti cha Syria baada ya rais Obama kuamua kupata ridhaa ya bunge la Marekani. Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaandika:

Kwa kuwa Obama anahisi analazimika kuingilia kati, ingawa asingependelea kufanya hivyo, ndio maana anaona bora angalao asake njia ya kupunguza athari zinazoweza kutokea bila ya kukusudiwa. Kwa kufanya hivyo amelenga zaidi siasa ya ndani kuliko Syria yenyewe. Warepublican wanamshambulia tu, mamoja anachokifanya au asichokifanya.Kwa kusaka ridhaa ya bunge la Marekani Congress, anawalazimisha waamue. Hatari kuliona bunge hilo likikataa kumuunga mkono, ni ndogo. Zaidi ya hayo anavuta wakati. Mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia, G20 mjini Moscow anaweza kushiriki bila ya kishindo cha hujuma za kijeshi. Na akibahatika pengine Putin akaregeza kamba.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo