1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu, Gordon Brown akosolewa vikali kutokana na matamshi yake

29 Aprili 2010

Uchumi: ndio mada kuu ya mjadala wa leo.

https://p.dw.com/p/N9QN
Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown akizungumza na mpiga kura. Brown alimtaja kama asiyewavumilia wengine.Picha: AP

Mjadala wa leo nchini Uingereza tayari umetajwa na wachunguzi wa maswala ya kisiasa kama kinyang’anyiro kikali na mada kuu ni masuala ya uchumi. Waziri mkuu Gordon Brown wa chama cha Labour, David Cameron wa chama cha kihafidhina, Conservative na Nick Clegg wa chama cha Liberal Democrat watakutana Birmingham kwa mjadala huo.

Waziri mkuu Gordon Brown anatarajiwa kutoa hoja nzito katika majadiliano hayo kwani aliwahi kuwa waziri wa zamani wa fedha.

Hata hivyo kashfa inayomkabili Bw. Brown kuhusu matamshi yake hapo jana kuhusu mwanamke mwenye umri wa miaka 66, Gillian Duffy kwamba ni mtu asiyewavumilia wengine, yamekuwa pigo kubwa na yamemsababishia kukosolewa na wengi humo. Tayari chama chake cha labour kipo katika nafasi ya pili na hata ya tatu katika kura tofauti za maoni nchini Uingereza.

Großbritannien Wahlen Sky news TV-Duell Gordon Brown, Nick Clegg und David Cameron
Waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, kulia, Nick Clegg, katikati na David Cameron, kushoto. Mjadala wa leo utafanyika Birmingham, UingerezaPicha: AP

Duffy aliuliza suali kuhusu uhamiaji, kodi na deni la serikali kabla waziri mkuu Gordon Brown kusikika akimfokea kutokana na kipaza sauti alichovaa ambacho alisahau kukizima.

Wapinzani na waandishi wa habari walimkemea Bw Brwon na gazeti linaloegemea siasa za mrengo wa shoto la Guardian liliyataja matamshi yake kama janga kubwa la kisiasa katika kampeni za mwaka wa 2010. Gazeti la The Sun lilisema Gordon Brown ni mwanasiasa mwenye matatizo ya kiakili ambaye kila mara hutaka kupata mtu wa kumlaumu

Msemaji wa masuala ya fedha wa chama cha kihafidhina cha Conservative, George Osborne alisema matamshi hayo ya Bw. Brown ni ya kutatanisha hasa ikilinganishwa na alichosema hadharani na lichonuia kusema faraghani. Hata hivyo Waziri mkuu,

Gordon Brown alikiri makosa yake na kuomba radhi.

Brown pia alituma ujumbe wa barua pepe kwa wakereketwa wa chama cha Labour na washirika wengine wa chama hicho akijaribu kuhimili tukio lililomkumba.

Hayo yamejiri wakati ikiwa zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi mkuu nchini Uingereza utakaofanyika tarehe 6 mwezi ujao.

Mwandishi, Peter Moss/ AFP/Reuters

Mhariri, Saumu Mwasimba