Mjadala kuhusu katiba mpya Uturuki
9 Januari 2017Katiba hiyo mpya , ambayo itakuwa badala ya sheria mama iliyotungwa baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Uturuki mwaka 1980, inataka kuweka kwa mara ya kwanza mfumo wa kirais kwa ajili ya kuliongoza taifa hilo la kisasa lililoundwa kutokana na mabaki ya himaya ya Ottoman.
Wakosoaji wamedai kwamba hatua hiyo ni sehemu ya uporaji wa madaraka unaofanywa na Rais Recep Tayyip Erdogan -- waziri mkuu wa Uturuki kuanzia mwaka 2003 hadi 2014 na baadaye rais , na kuiingiza nchi hiyo katika utawala wa mtu mmoja baada ya jaribio lililoshindwa la mapinduzi Julai mwaka jana.
Lakini Erdogan na chama chake tawala cha Justice and Development AKP wanasema mfumo wa kirais utaiweka Uturuki katika njia moja na mataifa mengine kama Ufaransa na Marekani na unahitajika kwa ajili ya serikali yenye ufanisi.
Mjadala huo kuhusiana na katiba hiyo mpya yenye sura 18 ulianza baada ya mswada huo kukubaliwa na tume ya bunge. Uwasilishaji wa mswada huo mara mbili unatarajiwa kukamilika mnamo siku 13 hadi 15.
Waandamanaji
Kundi dogo la waandamanaji lilijitokeza nje ya jengo la bunge mjini Ankara kabla ya mjadala wenyewe , lakini polisi walivunja maandamano hayo wakitumia maji ya pilipili dhidi ya waandamanaji.
Mmoja kati ya waandamanaji alilalamika baada ya polisi kulitawanya kundi lao kwa mabomu ya kutoa machozi.
"Uturuki imevamiwa. wale wanaohusika na miripuko, mapambano, silaha ni wale walioko madarakani hii leo. Kwa nini kunakuwa na ulinzi kiasi hiki, kuna vita vinavyoendelea hapa? Nataka kupita vizuwizi na kwenda mbele ya bunge lakini polisi hawataki kuniruhusu, wamejazana hapa. Kitu gani kinatokea katika nchi hii? Je kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe?"
Chama cha AKP kinahitaji zaidi ya kura 330 , tatu ya tano ya wingi kwa ajili ya mswada huo kuweza kufikishwa katika kura ya maoni ili kuidhinishwa na wapiga kura.
Katiba hiyo mpya inapingwa na chama kikuu cha upinzani , chama cha Republican Peoples Party CHP, ambacho naibu mwenyekiti wake Bulent Zezcan alisema itapeleka madaraka ikulu , yaliyochukuliwa kutoka Sultan wa enzi za Ottoman karne moja iliyopita.
Wakati huo huo rais Erdogan amesema leo kwamba anaamini mjadala kuhusu Uturuki na Marekani utashika kasi baada ya rais mteule Donald Trump kuingia madarakani na kwamba amjadiliano hayo yatafikia muafaka katika masuala ya kikanda. Uhusiano kati ya Marekani na Uturuki , washirika muhimu katika mapambano ya NATO dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq wameporomoka kwa kiasi kikubwa tangu jaribio lililoshindwa la mapinduzi ya kijeshi Julai mwaka jana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mahariri: Yusuf , Saumu