1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala 3 wa TV kabla uchaguzi wa Uingereza

30 Aprili 2010

David Cameroun ameshinda kwa hoja ?

https://p.dw.com/p/NAoS
Mjadala wa 3 wa TV Uingereza.Picha: AP

Mjadala wa tatu uliotuwama juu ya maswali ya uchumi -wiki kabla ya uchaguzi mkuu wa Uingereza, umempa mara hii ushindi wazi David Cameron, mtetezi mkuu wa chama cha Upinzani cha Conservative dhidi ya waziri mkuu, Gordon Brown, wa chama tawala cha Labour, ambae uchunguzi wa ghafula wa maoni , umemtupa nafasi ya 3 nyuma ya Nick Clegg wa chama kidogo cha Liberal Democrat.

Kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani Conservative Party, David Cameron, ameamua kutumia ushindi wake kutoka mjadala wa jana usiku katika TV kukipiga jeki chama chake kunyakua ushindi wazi katika uchaguzi ujao wa Bunge alhamisi ijayo (Mei 6).

Wiki tu ikisalia kabla ya kura kupigwa, uchunguzi wa ghafula wa maoni kutoka kwa watazamaji, umeonesha Kiongozi wa Conservative party, David Cameron, ndie alietoa hoja nzito na mshindi wa duru hiyo ya tatu.Kiongozi wa chama cha Kiliberali, Nick Clegg, aliibuka wa pili wakati waziri-mkuu Gordon Brown (Labour) ametokea wa mwisho.

"Msipoteze wakati hata dakika moja wala saa moja, nchi hii imechoka na inalilia mabadiliko. Inatupasa kuwafahamisha wananchi kwamba, njia pekee ya kufikia mabadiliko hayo ni kukichagua chama cha Conservative."Alisema David Cameron.

Katika mjadala huo, Gordon Brown, waziri wa fedha kwa mwongo mzima kabla kumrithi Tony Blair, wadhifa wa uwaziri mkuu mwaka 2007, aliungama makosa yake.

"Wadhifa huu una majukumu mengi na kama mlivyojionea jana, sio kila mara sifanyi makosa." -Alisema waziri mkuu Brown, mwanzoni mwa mjadala huo.

Aliongeza lakini kusema,

"Hata hivyo, ninaelewa vipi kuongoza uchumi unapostawi, lakini pia unapokubwa na misukosuko. Pale mabenki yalipoporomoka, nilichukua hatua haraka kupambana na msukosuko ili usigeuke msiba na hali ya kuzorota uchumi isigeuke kupooza uchumi."

Kiongozi wa chama cha Conservative, David Cameron, anajaribi kuepusha kupanga maafikiano yoyote wakati huu na Nick Clegg , kiongozi wa chama kidogo na cha tatu katika mbio hizi za kuelekea Ikulu (10 Downing Street). Anapigania kujipatia wingi wa viti katika bunge la viti 650 ili kuweza kutawala pekee bila ya kubidi kuunda serikali ya muungano na Liberal Democrat.

Kituo cha kuagua cha mtandao ( Bettfair) kimesema uwezekano wa chama cha Conservative sasa kujipatia wingi wa kutawala pekee ,umeongezeka kwa pointi 3.

Bw.Cameron, alikosoa rekodi ya uendeshaji uchumi ya waziri mkuu Gordon Brown, na akachora picha ya hofu ya Uingereza kufuata nyayo za pale Ugiriki ilipofikia hivi sasa.

Chama cha Labour cha waziri mkuu Brown, kinadai kubana matumizi sasa si sawa na ingefaa kusubiri hadi kwanza uchumi umestawi barabara. Brown amesema, paparapara za chama cha Conservative kubana matumizi kutaitosa tena Uingereza katika hali iliokuwapo kabla ya kuzorota uchumi wake, hali ambayo ndio kwanza imejikomboa.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Uhariri: Miraji Othman