Mizozo, majanga yaongeza wakimbizi wa ndani Barani Afrika
26 Novemba 2024Mkuu wa Taasisi ya kimataifa inayoangazia Wakimbizi wa Ndani, IDMC Alexandra Bilak ameliambia shirika la habari la AFP baada ya kuchapisha ripoti hii leo Jumanne kwamba, idadi hiyo ni karibu nusu ya watu walioyakimbia makazi yao ulimwenguni.
Amesema wameshuhudia idadi hiyo ya Afrika ikiongezeka mara tatu zaidi ya watu walioyakimbia makazi yao kote ulimwenguni katika kipindi cha miaka 15 iliyopita na kuongeza kuwa wengi wao wanakimbia kutokana na mizozo, machafuko lakini pia majanga, ambayo sasa yanaonekana kuchochea hata zaidi tatizo hilo.
Ripoti hii inaonyesha kuongezeka kwa viwango vya mizozo na machafuko kumesababisha watu milioni 32.5 kuyakimbia makazi yao, asilimia 8 miongoni mwao wakiwa wamekimbia katika mataifa matano ambayo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Nigeria, Somalia na Sudan.
Kulingana na Bilak, idadi ya watu waliolazimika kuondoka kwenye makazi yao kutokana na majanga na hasa mafuriko pia inaongezeka barani Afrika. Idadi hiyo imeongezeka mara sita kati ya mwaka 2009 na 2023, kuanzia watu milioni 1.1 kwa mwaka hadi milioni 6.3.
Soma pia: Watu zaidi ya 700,000 wakimbia machafuko Haiti
Mafuriko yalisababisha zaidi ya robo tatu ya watu kuondoka, na asilimia 1.1 waliimbia hali ya ukame.
Mkataba wa Kampala bado haujasaidia kupunguza tatizo
Kufuatia ripoti hiyo, Taasisi hiyo imeuangazia Mkataba wa Kampala wa Umoja wa Afrika wa kulinda na kuwasaidia wakimbizi wa ndani, kama nyenzo muhimu ya kushughulikia tatizo hilo.
Mkataba huo, ulioidhinishwa mwaka 2009 na kuanza kutumika Disemba 2012, uliweka kiwango cha kimataifa kama cha kwanza, na ambacho bado ni makubaliano pekee ya kikanda yenye uzito wa kisheria kushughulikia wakimbizi wa ndani.
Nchi 34 za Afrika zimeidhinisha mkataba huo, huku nyingi zikitengeneza mifumo ya kisheria na kufanya uwekezaji mkubwa kushughulikia suala hilo. Lakini IDMC imesema ingawa serikali zilijitahidi kupambana, lakini juhudi hizo zilidhoofishwa na ongezeko la migogoro na majanga, yaliyochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Bilak amesema hii inamaanisha kwamba bado makubaliano hayo hayajaweza kuleta suluhu. Akasema, wakati wengi wakikimbia kutokana na mizozo barani Afrika, bado kuna mengi ya kufanywa, linapokuja suala la kujenga amani, diplomasia na mchakato wa kuweka mifumo ya amani kwenye maeneo yenye mizozo.
Soma pia:Mzozo wa Sudan wasababisha maelfu kuyakimbia makazi yao