1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mitandao ya kijamii kwenye uchaguzi Tanzania

Elizabeth Shoo18 Oktoba 2015

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, vyama vya siasa vya Tanzania vinatumia mitandao ya kijamii kufikisha taarifa na matangazo moja kwa moja kwa wapiga kura. Hivyo kampeni zimepata sura ya tofauti.

https://p.dw.com/p/1Gq34
Twitter na Facebook
Picha: Reuters

Kama wewe ni raia wa Tanzania mwenye simu ya mkononi bila shaka katika siku zilizopita umekuwa ukitumiwa ujumbe mfupi ama picha zinazohusiana na wanasiasa ama vyama fulani. Moja ya mitandao iliyotumika sana wakati wa kampeni ni mtandao wa WhatsApp kwenye simu za mkononi za kisasa. "Unakuta mtu anapopata taarifa na kuzithibitisha, anazituma kwenye kundi moja la WhatsApp. Kama hilo kundi lina watu 100, wao pia wanazituma kwa marafiki zao. Ndani ya dakika 20 unakuta taarifa imeshaenea Tanzania nzima kwa sababu ya mtandao," anasema Nchang'wa Nhumba, mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Tanzania. Kuna aina mbali mbali za ujumbe wa kampeni. Mara nyingi unakuta ni picha inayoambatana na maneno, ambapo aidha mgombea kama Edward Lowassa ama John Magufuli anapigiwa debe, au kinyume chake unakuta mashabiki wa chama kimoja wanasamabaza picha, maneno ama video za kuwapaka matope wapinzani wao.

Kwa mfano katika mtandao wa Twitter, mashabiki wa CCM wamekuwa wakisambaza video hii ambapo mtu anagusia Magufuli alipopiga "push up" kwenye kampeni. Na hapa anasema ingekuwaje kama Magufuli na Lowassa wote wangeambiwa wapige "push up" tano.

Lakini upande wa upinzani nao hauko kimya:

Video ifuatayo ya wanaomuunga mkono Lowassa imesambazwa sana kwenye WhatsApp na ipo pia YouTube:

Vyama vya kisiasa mwaka huu vimehakikisha kuwa vinatumia fursa zote ambazo mtandao unatoa, kwani ni chombo kinachowezesha kufikishia watu ujumbe haraka. Ndio maana vyama vyote vina akaunti rasmi kwenye mitandao kama Twitter ambapo mtumiaji anapata habari zote muhimu: "Kuna taarifa nyingi za kampeni zinazotoka kwenye vyama na kusambazwa kwenye mitandao," anasema Ben Taylor, mchambuzi ambaye amekuwa akifuatlia siasa na vyombo vya habari nchini Tanzania kwa muda mrefu. "Wakati mwingine taarifa hizo zinasambazwa na akaunti rasmi za vyama au na watu wanaounga mkono vyama fulani au wanasiasa fulani. Nadhani baadhi yao wanalipwa kufanya hivyo, lakini wengine wanafanya tu kwa sababu wanakiunga mkono chama."

Hata hivyo, inafahamika kwamba mitandao ina hatari zake, kwani si rahisi kuthibitisha uhalisia wa picha, video na ujumbe unaotumiwa kwenye simu yako. Baadhi ya vyama vimeshutumiwa kutumia programu za kompyuta ili kuongeza idadi ya watu wanaoonekana kwenye picha za mikutano ya kampeni, ili kuashiria kwamba mgombea fulani ana mashabiki wengi sana. Mchambuzi Ben Taylor anatoa maelezo zaidi kuhusu WhatsApp: "Watu wanafeki chati za whatsapp wakitaka kuwaaibisha wapinzani wao. Utakuta mwanasiasa anafeki chat ya whatsapp ambayo inaonyesha kuthibitisha uvumi kuhusu mpinzani wake na kuusambaza ujumbe huo kwenye mitandao ya kijamii. Na watu ni wepesi sana kuamini ujumbe wa aina hiyo." Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, mara nyingi watu wakiona picha inayoonyesha wanasiasa wawili wakibadilishana maneno kwenye WhatsApp, wanaamini kuwa kweli wanasiasa hao walikuwa wanachat, licha ya kwamba ni rahisi sana kughushi picha ili ionekane kama chat ya WhatsApp.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Dahman