Misri yatuhumiwa kuwakandamiza wapinzani
27 Novemba 2019Shirika la kutetea haki za binadamu la kimataifa Amnesty International limetowa ripoti inayosema kwamba serikali ya Misri inatumia shirika maalum la siri la usalama,ambalo liliundwa kupambana na ugaidi,kuwakamata waandamanaji,waandishi habari na wakosoaji wa serikali hiyo.
Ripoti iliyotolewa na shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza imetowa maelezo ya kina juu ya vipi shirika lisilotambulika sana la kiusalama lililoundwa na serikali ya Misri linaloitwa SSSP lilivyokuwa kiini cha kuongezeka hatua kamatakamata iliyoanzishwa na rais Abdel Fatah El Sisi dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake.
Shirika kuu la usalama wa dola na uendeshaji mashtaka kama linavyoitwa limetanua suala zima la maana ya ugaidi na kuwalenga hadi watu wanaoshiriki maandamano ya amani, wanaotuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na hata wanaofanya shughuli halali za kisiasa.
Hivyo ndivyo anavyosema Phillip Luther ambaye ni mkurugenzi wa Amnesty International tawi la Mashariki ya kati na Afrika Kaskazini Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo hata watu wanaokwenda kuhudhuria matamasha walituhumiwa kuwa magaidi kwa kupeperusha bendera iliyokuwa na rangi mchanganyiko za Rainbow.
Kuna mwandishi habari aliyeshtakiwa kwa kile kilichoitwa kutangaza habari za uwongo na alizuiliwa jela mara kadhaa kwa kipindi cha miaka mitatu. Wakili mmoja anayetetea haki za binadamu naye alikamatwa kwa kujiunga na maandamano ambayo binafsi anasema hakushiriki.
Kuna wakristo chungunzima waliofungwa kwa kile kinachoitwa kulisaidia kundi la kigaidi: Kundi linalokusudiwa hapo ni kundi la Udugu wa Kiislamu au Muslim Brotherhood. Mwandishi wa ripoti hii ya Amnesty International Hussein Baoumi anasema Mashataka yote ni kichekesho na ni ya kutungwa.
Kwa kutowa mifano hiyo na mamia ya kesi nyinginezo,Amnesty International linasema SSSP shirika ambalo linaendesha shughuli zake kwa siri na kusimamiwa na majaji wachache wa kuteuliwa linatumia vibaya mamlaka yake ya kisheria kama tawi lililoundwa kwa nia ya kupamabana na ugaidi,ambalo sasa limegeuka kuwa fimbo dhidi wapinzani wakisiasa. Baoumi anasema kuna tatizo la kimahakama, na taasisi hiyo imezunguukwa na usiri.
Kwasababu ikiwa kesi hizi zote zingepelekwa mahakamani na watu kusimamishwa kizimbani basi watu hawa wangeachiliwa huru mara moja kwasababu tuhuma zinazotolewa na serikali zinatokana na ripoti za siri za polisi. Ripoti ya Amnesty international pia inasema wachunguzi wa tawi la SSSP kuhusu tuhuma za kuhusishwa polisi na utesaji pamoja na watu kupotea wamekuwa wakihusika kuuzika ushahidi wa vitendo hivyo vya polisi na kuonesha sura tafauti ya mambo. Kadhalika ripoti hiyo inasema chini ya El Sisi Misri imeshuhudia kuongezeka kwa kasi kubwa vitendo vinavyosimamiwa na SSSP. Wiki hii tu polisi iliwakamata watu sita wakiwemo waandishi habari watatu mjini Cairo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo