1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yapendekeza kusitishwa mapigano kwa siku mbili Gaza

28 Oktoba 2024

Misri imependekeza makubaliano ya siku mbili ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza. Nchini Lebanon watu watano wameuawa katika shambulio la Israel lililolenga katikati mwa jiji la Tyre

https://p.dw.com/p/4mJ13
Ägypten | Präsident Abdel Fattah El-Sisi
Picha: Jacquelyn Martin/Pool/AP Photo/picture alliance

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amependekeza mpango wa kusitisha mapigano kwa muda wa siku mbili katika Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka wachache huku malengo ya kufikiwa usitishaji kamili wa mapigano kati ya Israel na Hamas yakiendelea kufanyiwa kazi.

Katika pendekezo hilo lililotolewa hapo jana Jumapili mateka wanne wa Israel kati ya mateka wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza wataachiwa huku Israel nayo inatakiwa iwaachie wafungwa wa Kipalestina walio katika jela za Israel. Rais wa Misri amesema mazungumzo zaidi yatafanyika ndani ya siku 10.

Misri | Rais wa Misri  Abdel-Fattah al-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah al-SisiPicha: THIBAULT CAMUS/AFP via Getty Images

Hata hivyo, Rais wa Misri hakueleza iwapo mpango huo tayari umeshawasilishwa kwa Israel au kwa Hamas. 

Soma Pia: Umoja wa Mataifa wasema hali ya Gaza ni giza zito 

Mapendekezo ya rais wa Misri yametolewa wakati Israel ikiendelea kulivamia eneo la Wapalestina, na pia inaendeleza vita vyake dhidi ya kundi la Hezbollah nchini Lebanon na wakati huo huo, imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya hasimu wake mkuu Iran.

Nchini Lebanon wizara ya afya imesema majeshi ya Israel yameushambulia mji wa kusini wa Tyre hii leo Jumatatu, takriban watu watano wameuawa na wengine 10 wamejeruhiwa.

Tyre, mji wa kale wa pwani ambao umeorodheshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kuwa ni eneo la Turathi ya Dunia, ulikumbwa na mashambulizi makali ya Israel wiki iliyopita, yaliyosababisha uharibifu mkubwa katika maeneo mengi ya mji huo wa kale.

Wakati huo huo, Kamanda mwandamizi wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran ameionya Israel kuwa itakabiliwa na "madhara makubwa" baada ya nchi hiyo kuyashambulia  maeneo ya kijeshi ya Iran.

Rais wa Iran Maoud Pezeshkian
Rais wa Iran Masoud PezeshkianPicha: Dolat.ir

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema nchi yake itaendelea kusimama imara hata baada ya mashambulizi ya Israel na kamwe haitarudi nyuma.

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema "Tehran, itatumia zana zote zilizopo" kujibu mashambulio ya Israeli ya mwishoni mwa wiki yaliyolenga vituo vya kijeshi nchini humo ingawa awali iliyapuuza mashambulizi hayo ya anga ya Israel ikisema yalisababisha uharibifu mdogo tu. Rais wa Marekani Joe Biden alitoa wito wa kuepuka kuongeza mivutano kati ya pande hizo mbili ambayo imezua hofu ya uwezekano wa kutokea mzozo mkubwa katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Soma Pia: Umoja wa nchi za kiarabu wasisitiza kusimamishwa mapigano Lebanon 

Iraq imelaani kutumiwa anga yake na Israel katika kuishambulia nchi jirani ya Iran. Msemaji wa serikali ya Iraq Bassim Alawadi. Amesema nchi yake imewasilisha barua ya malalamiko kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Alawadi amesema wizara ya mambo ya nje ya Iraq pia italileta swala hili la ukiukaji wa anga yake katika mazungumzo na Marekani, mshirika wa karibu wa Israel na mtoaji mkuu wa silaha kwa taifa hilo.

Vyanzo: AFP/RTRE