Misri yalipa kisasi dhidi ya Ghana
14 Novemba 2016Katika bara la Afrika , Misri ililipa kisasi kipigo cha kudhalilisha katika mchezo wa kombe la dunia dhidi ya ghana miaka mitatu iliyopita kwa kuishinda timu hiyo Black Stars kwa mabao 2-0 jana Jumapili ambapo mashabiki 85,000 walishuhudia pambano hilo mjini Alexandria.
Ghana ilishinda kwa mabao 6-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa wa kombe la dunia mwaka 2014 na ushindi huo uliendeleza maumivu ya Misri , ambayo haikushiriki katika fainali za kombe la dunia tangu mwaka 1990.
Ghana ambayo inawania kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia kwa mara ya nne mfululizo , ilitawala kipindi cha pili bila ya kuweza kupata njia ya kumfikia mlinda mlango mwenye umri wa miaka 43 Essam El Hadary.
Katika michezo mingine Guinea iliangukia pua pale ilipolazwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo jana Jumapili na Tunisia iliibuka kidedea dhidi ya Algeria kwa ushindi wa bao 1-0.
Kocha wa timu ya taifa ya Afrika kusini Ephraim Mashaba amesitishwa kazi na chama cha kandanda nchini humo baada ya kuhusika katika mvutano na maafisa kufuatia ushindi wa timu hiyo katika kombe la dunia dhidi ya Senegal mwishoni mwa juma.
Mashaba atakosa kuwapo katika benchi la ufundi la timu hiyo Bafana Bafana kesho Jumanne dhidi ya Msumbiji na anakabiliwa na kikao cha nidhamu kuhusiana na madai ya tabia ya kiburi dhidi ya rais wa shirikisho la kandanda nchini Afrika kusini SAFA Danny Jordaan na wageni wake, ambao walikwenda kuipongeza timu katika vyumba vya kuvalia baada ya ushindi wa mabao 2-1 siku ya Jumamosi dhidi ya Senegal mjini Polokwane.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Yusuf Samu