Misri: Ukandamizaji waendelea licha ya kuachiwa wanaharakati
22 Julai 2021Mapumziko ya wiki hii ya sherehe ya Eid al-Adha yalileta habari njema kwa karibu wafungwa 40 katika magereza ya Misri, kwamba walikuwa huru kuondoka, miongoni mwao wakiwemo waandishi habari mashuhuri watatu na wanaharakati watatu wa haki za binadamu.
Lakini kuachiwa kwao hakumaanishi bado kwamba wameondolewa makosa. Wote 40 watafika tena mahakamani baadae mwaka huu.
Moja wa walioachiwa ni Esraa Abdel-Fattah, mwanablogi maarufu anaejulikana kama Msichana wa Facebook. Esraa mwenye umri wa miaka 43 na mteule wa tuzo ya amani ya Nobel amekaa gerezani kwa takribani miaka miwili kwa kosa la kueneza kile serikali inachokiita habari za uzushi na mashtaka ya kuipinga serikali.
Mwingine alieachiwa ni mwandishi habari anaeukosoa utawala Gamal el-Gamal, alieishi nchini Uturuki kwa miaka minne, akiendesha kipindi cha Televisheni na mashughuli pia kwenye mtandao wa Facebook. Alipelekwa rumande mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Cairo mapema mwaka huu.
"Nakaribisha kwa dhati kuachiwa kwa hivi karibuni, wawili kati ya yalioachiwa ni watu ambao nimewafahamu binafsi kwa zaidi ya muongo mmoja. Naweza kukuambia namna nilivyofurahi, lakini pia nina imani pia kwamba hili siyo suluhisho la kudumu.
Ni sahihi, nimefurahi kwamba tumewatoa watu hawa, lakini kuna wengi zaidi ndani," alisema Ramy Yaacoub, mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya sera ya Mashariki ya Kati mjini Washington, Marekani.
Kuachiwa kwafunikwa na ukandamizaji
Kuachiwa hivi karibuni kwa wanaharakati na waandishi habari kunatofautiana kabisaa na ukandamizaji unaoendelea nchini Misri. Wiki hii mhariri mkuu wa zamani wa gazeti la kila siku la Misri la Al-Ahram, Abdel Naser Salama, alishikiliwa kwa madai ya ugaidi na habari za uongo.
Soma pia: Macron akosolewa kumkaribisha rais al-Sisi wa Misri
Wiki iliyopita, kesi katika mahakama ya juu kabisaa ya Misri, iliendelea dhidi ya wanaharakati na waandishi habari sita, akiwemo mbunge wa zamani Zyad el-Elaimy.
Misri pia haina huruma kwa wanachama wa kundi la Udugu wa Kiislamu, ambalo liliorodhesha kuwa kundi la kigaidi mwaka 2013. Juni mwaka huu, hukumu ya kifo dhidi ya wananchama 12 wa Misri ilishiikiliwa. Familia zao sasa zimeanza kampeni ya mitandao ya kijamii chini ya Hashtag ya #StopEgyExecutions, ili kuoinga hukumu hizo na kuvuta nadhari.
Mmoja waliotiwa hatiani ni Mohamed El-Beltagy, aliekuwa mashuhuri katika mapinduzi ya Misri ya 2011. Mke wake Abd Al-Gawad, ameandika barua, ambayo DW ilipata nakala yake. Katika barua hiyo, anautuhumu utawala wa Misri kwa kuwanyima haki za msingi za binadamu wafungwa.
Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch linakadiria kuwa takribani watu 60,000 wako korokoroni nchini Misri kwa sasa kwa sababu za kisiasa.
Taifa hilo pia liliongoza orodha ya Amnesty International, ya mataifa yalio na hukumu nyingi za kifo na mauaji katika mwaka 2020. Tarakimu za Misri ziliongezeka zaidi ya maradufu kutoka 32 mwaka 2019, hadi 107 mwaka uliofuata.
Wasiwasi wa wazi kutoka Washington
Ukamataji na hukumu za karibuni zimevutia nadhari -- juu ya yote kutoka mshirika wa Misri mwenye nguvu Marekani.
Wiki iliyopita, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Ned Prince, alielezea wasiwasi kuhusu hatia ya Misri iliyochochewa kisiasa dhidi ya Hossan Bahgat, mwandishi mashuhuri wa habari za uchunguzi na mkurugenzi mkuu wa shirika la Haki Binafsi la Misri (EIPR).
Soma pia: Rais wa zamani wa Misri Morsi azikwa baada ya kufariki mahakamani
Prince alisema katika mkutano na waandishi habari kwamba Marekani haitapuuzia haki za binadamu kwa kisingizio cha usalama, utulivu au maslahi yoyote inayoweza kuwa nayo nchini Misri.
Moha,ed El Dahshan, msomi kutoka programu ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ya taasisi ya Chatham House, anasema shinikizo la kimataifa linaweza kumfanya rais Abdel-Fattah el-Sissi na serikali ya Misri kubadili tabia zao, lakini akaongeza kuwa ukweli ni kwamba hakuna aliejaribu hilo kwa uzito.
Yaacoub anaona njia nyingine za kuishawishi Misri kuisikiliza Marekani, kwa mfano katika mzozo wake na Ethiopia kuhusu bwawa la umeme linalojengwa kwenye Mto Nile, au kupitia mikopo ya elimu na programu zinazoweza kutolewa au kutumiwa katika mkakati huo.
Kwa kiwango chochote, inasalia kitendawili kuona iwapo Cairo itageuza haki za binadamu kuwa alama yake mpya - au iwapo watu watu walioachiwa hivi karibuni wanaonekana kama jambo la kipee tu lililosababishwa na mapumziko ya kila mwaka ya Eid.
Waandishi: Jennifer Hollesi, Kersten Knipp /DW Mashariki ya Kati