Misaada yaanza kuwasili Ufilipino
15 Novemba 2013Katika mji wa Merida uliopo kisiwani Leyte , taka bado zimezagaa barabarani kutokana na mabaki ya majengo yaliyoporomoka.
Kimbunga Haiyan kimeshambulia mno katika eneo hilo. Takriban wiki moja baada ya kimbunga hicho wakaazi wa mji wa Merida wameanza kazi ya ujenzi mpya na baadhi ya nyumba zimeanza kutumika. Mvua bado inaendelea kunyesha na wakaazi wa mji huo hujikusanya pamoja katika nyumba ambazo zimebakia na paa juu yake na zile ambazo zimeanza kujengwa na wanajihifadhi kwa pamoja.
Juhudi za kuwasaidia watu walionusurika na kimbunga Haiyan nchini Ufilipino zimeongezeka kuanzia leo, licha ya kuwa serikali imekiri kuwa kasi yale bado ni ndogo.
Waziri wa mambo ya ndani Mar Roxas amesema kuwa katika mji wa Tacloban , mji mkuu wa jimbo lililoathirika kwa kiasi kikubwa la Leyte, malori yaliyobeba mahitaji mbali mbali yamefika katika miji 30 kati ya 40 katika jimbo hilo.
Usafishaji waanza
Wafanyakazi wakiwa na misumeno ya umeme wamekuwa wakikata miti iliyoanguka mjini Tacloban wakati malori yakibeba miili ya watu waliofariki pamoja na taka zilizozagaa mitaani, na wengine wakikarabati nyumba zilizoporomoka.
Rais Benigno Aquino, ameshindwa kutambua ukubwa wa maafa hayo, na amekosolewa kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa misaada pamoja na makadirio yenye utata ya watu waliofariki, hususan katika mji wa Tacloban, mji ambao umeathirika mno na kimbunga hicho.
Meya aomba radhi
Taarifa katika jengo la halmashauri ya mji wa Tacloban imekadiria kuwa watu 4,000 wamefariki , ikiwa ni ongezeko kutoka idadi ya watu 2,000 waliotangazwa siku moja kabla katika mji huo pekee. Hata hivyo meya wa Tacloban Alfred Romualdez aliomba radhi na kusema kuwa idadi hiyo ni kwa eneo lote la kati la Ufilipino.
Waziri wa mambo ya ndani Mar Roxas amesema kuwa juhudi za kutoa misaada zinaendelea, licha ya kuwa kasi yake ni ndogo bado. Amesema kuwa kila siku inakuwa bora zaidi kuliko siku iliyopita. Haiwezekani kasi kuwa kubwa katika hali kama hii kwasababu watu wengi mno wameathirika na miundo mbinu imeharibika.
Sandra Bulling kutoka katika shirika la kutoa misaada la Care International amesema misaada imeanza kuwafikia walengwa.
"Kwa hivi sasa misaada yetu ya chakula imo njiani kutoka Manila kuja hapa kisiwani. Misaada hiyo itawasili kesho na tutaweza haraka iwezekanavyo kugawa misaada katika eneo la Mormoc. Na mpango ni kwamba katika muda wa siku chache zijazo tutaweza kutumia fursa hii, kufikisha misaada hiyo Merida ama Isabel. Na katika siku chache zijazo tutaleta vifaa vya ujenzi, ili watu waweze kupata mahali pa kuishi."
Lakini wakati juhudi za kutoa misaada zikiendelea , wataalamu kutoka shirika la afya ulimwenguni WHO pamoja na mashirika mengine yamerudia ushauri wao kuwa serikali ya Ufilipino inapaswa kulenga juhudi zake za kutoa misaada kwa watu walionusurika, badala ya kushughulikia waliofariki.
Mwandishi: Peter Hille / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Daniel Gakuba