1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaLibya

Misaada yaanza kuwasili Libya kusaidia manusura wa mafuriko

16 Septemba 2023

Misaada ya kimataifa imeanza kuwasili nchini Libya leo kutoa ahueni kwa walioathiriwa na janga la mafuriko makubwa ambayo pia yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuleta uharibifu usio na mfano.

https://p.dw.com/p/4WQLY
Mji wa Derna baada ya janga la mafuriko
Mafuriko yameharibu kabisa mji wa Derna Picha: TUR Disaster & Emergency Management/AA/picture alliance

Mafuriko hayo ya Jumapili iliyopita kwenye mji wa bandari wa Derna, yaliwasomba watu na makaazi yako kuelekea baharini baada ya kingo za mabwawa makubwa mawili kupasuka kutokana na mvua kubwa iliyosababishwa na kimbunga cha bahari ya Mediterrania.

Hii leo ndege mbili za shehena ya misaada moja kutoka Umoja wa Falme za Kiraabu na nyingine ya Iran zimetua mjini Benghazi, kiasi kilometa 300 magharibi mwa Derna. Shehena hiyo itasombwa kwa malori kwenda kwenye mji huo ambako juhudi za kuwatafuta watu waliotoweka  zinaendelea bila ya matumaini ya kupatikana manusura.

Hadi sasa takwimbu za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa zinasema miili ya watu 3,958 imepatikana na kutambuliwa na rikodi zinaonesha watu wengine 9,000 hawajulikani waliko.