1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya kibinadamu yawasili Lebanon

Zainab Aziz22 Mei 2007

Msafara wa magari ya kupeleka misaada umewasili katika kambi ya Wapalestina ya Nahar al Bared huko kaskazini mwa Lebanon ili kugawa misaada ya dharura iliyokuwa inahitajika baada ya mapigano mabaya ya siku tatu.

https://p.dw.com/p/CB41
Moshi wafuka katika kambi ya wakimbizi ya Nahr al_Bared
Moshi wafuka katika kambi ya wakimbizi ya Nahr al_BaredPicha: AP

Shirika la kutoa misaada la umoja wa matiafa lilifanikiwa kufikisha malori manne yaliyosheheni chakula, madawa na majenereta katika kambi hiyo ya wakimbizi wa Kipalestina ameeleza msemaji wa shirika hilo.

Hayo yamewezekana baada ya wapigananaji wa kiislamu waliohusika katika vita vikali vya siku tatu kati yake na majeshi ya Lebanon kutangaza kuwa wata simamisha vita hivyo kwa muda kwa ajili ya kuitikia vilio vya raia waliojikuta wamekwama kutokana na vita hivyo.

Mashirika ya kutoa misaada yalipaaza sauti kwamba kambi hiyo itakabiliwa na maafa ya kiutu.

Wakimbizi katika kambi hiyo walikabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula, madawa na maji safi ya kunywa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa nguvu za umeme.

Mkurugenzi wa shirika la umoja wa mataifa la kuwasaidia wakimbizi wa Palestina bwana Richard Cook anahofia hali hiyo mbaya kuwa inaweza kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu.

Na hali ya mivutano ina maana kuwa raia wa kawaida ndio wanaumia zaidi.

Takriban wakimbizi wa Kipalestina 367,000 wanaishi katika hali duni kwenye kambi 12 nchini Lebanon.

Amri ya kusimamisha mapigano kwa muda imeanza kufanya kazi leo mchana ili kutoa fursa ya kuwasafirisha majeruhi na pia kuruhusu kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi, hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa kundi la Fatah al Islam Abu Selim aliyezunguza kwa njia ya simu na shirika la habari la hapa Ujerumani la DPA.

Amesisitiza kuwa mapigano hayo yamesimamishwa kwa muda tu.

Kwa upande wake jeshi la Lebanon limesema kwamba halitafyatua risasi ila pale litakaposhambuliwa.

Takriban watu 66 wameuwawa katika mapigano hayo baina ya majeshi ya serikali na kundi la waislamu wenye msimamo mkali huko kaskazini mwa Lebanon.

Mapigano hayo ni makubwa zaidi kuwahi kutokea ndani ya Lebanon tangu kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975 hadi mwaka 1990.

Mapigano hayo katika kambi ya wakimbizi ya Nahr al Bareh yamepingwa vikali na wakimbizi wa Kipalestina walio katika kambi jirani ya Bedawi ambao wamelaani kuuwawa kwa Wapalestina wenzao wasio na hatia.

Wakimbizi wa Kipalestina walio katika kambi ya Ain al Hilweh karibu na mji wa bandari wa Sidon, kusini mwa Lebanon wameandamana kupinga mapigano hayo.

Chama kikuu cha Fatah kimesema idadi ya wakimbizi wa Kipalestina katika maeneo mengine nchini Lebanon huwenda ikaongezeka iwapo wanajeshi watendelea kuishambulia kambi ya Nahr al Bared.

Mkuu wa sera za mambo ya nje wa umoja wa umoja wa Ulaya Javier Solana amewasili mjini Beirut kwa mazungumzo na utawala wa Lebanon kuhusiana na mapigano hayo.