1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko kutoka kwenye jua yawatisha watafiti

9 Juni 2011

Wanasayansi wanasema kwamba muangaza mkali ulioonekana kwenye anga hivi karbuni, ni nyota kubwa za zamani ambazo zinaweza kuathiri mawasiliano na nishati katika sayari ya dunia katika siku za karibuni.

https://p.dw.com/p/11XSj
Picha ya NASA inayoonesha miripuko kutoka kwenye jua
Picha ya NASA inayoonesha miripuko kutoka kwenye juaPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa za karibuni kabisa kutoka duru za kisayansi zinaonesha kwamba muangaza huo mkali sana, ambao baadhi ya wakati unang'ara zaidi kuliko jua la kawaida, unatoka kwenye nyota sita kongwe.

Hapo juzi (Jumanne, 07 Juni 2011), NASA iliripoti kwamba nyota hizi hazitakuwa na athari kubwa kwa sayari ya dunia, zaidi ya kutengeneza wingu ambalo lilifunika jua kwa zaidi ya nusu hapo Jumanne.

Lakini taarifa za jana zinasema kwamba hali huenda isiwe kama ilivyotarajiwa hapo mwanzoni. Robert Quimby wa Taasisi ya Teknolojia ya Carlifornia, ambaye ndiye aliyeongoza utafiti juu ya kutokea kwa miripuko ya ajabu, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kinachotokezea sasa "ni kitu kipya ambacho bado hakijaweza kupatiwa maelezo kwa vipimo vilivyopo".

Kwa kawaida, muangaza mkali kama huu hutokezea kutoka angani pale nyota kubwa zinapoishiwa na mafuta, kugongana na kuripuka na kuacha nyota ambazo hazina nishati au shimo jeusi.

Jua lilipopatwa mwezi Aprili 2011, nchini Ujerumani
Jua lilipopatwa mwezi Aprili 2011, nchini UjerumaniPicha: dapd

Pia kunakuwa na aina nyengine ya nyota, zinazoitwa nyota nyekundu, ambazo hupoa nishati yake kutokana na ukongwe na kuwa nyeupe, ambapo hali ya joto na uzito wake hugongana na kusababisha miripuko.

Lakini miripuko hii sita iliyochunguzwa na timu ya Robert Quimby haikuwa na aina ya kemikali zinazojuilikana kikawaida. Dokta Klaus Börger wa Kituo cha Taarifa za Sayari cha Ujerumani, anasema kwamba hata kama hakujawa na athari ya moja kwa moja kwa sasa, muangaza huu mkali kutoka angani unaweza ukaiathiri vibaya sayari ya dunia.

"Hizi ni chembechembe halisi za elektroni na protoni. Zinaonekana ikitoka kwa kasi kutoka kwenye jua kuelekea kwenye sayari ya dunia. Hilo linaweza kupelekea mkorogano wa kimawasiliano kwenye sayari ya dunia, ingawa bado mtu hawezi kutabiri kuwa muangaza huo utatua hasa juu ya uso wa dunia au kando kando." Anasema Dk. Börger.

Muangaza huu mkali una joto kali sana, kiasi ya nyuzi joto 20,000, na unatembea kwa kasi kilomita 10,000 kwa sekunde. Na pia unachukua kiasi ya siku 50 kufifia, ikiwa ni muda mrefu zaidi kulinganisha na iliyowahi kutokea hapo nyuma, ambayo ilichukua siku au wiki chache tu.

Lau ukifika kwenye uso wa dunia kwa kasi na ukali wake huu huu, muangaza huu mkali unatishia kutibua mawasiliano kupitia satelaiti, kama vile rada zinazotumia mfumo wa GPS, simu za mikononi na mawasiliano ya mtandao wa intaneti.

Eneo jengine linaloweza kuathirika haraka na moja kwa moja ni umeme unaotokana na nishati ya jua. Katika jimbo la Quebec, huko Canada, karibuni wakaazi milioni sita walijikuta wakiwa kwenye giza kwa muda. Dk. Börger anasema hili ni jambo linalotarajiwa katika hali kama hii.

"Tunahofia sana suala la umeme. Maana umeme unategemea na kani ya usumaku. Wakati pande mbili za sumaku na umeme zinapogusa ardhi, kinachotokea ni mabadiliko makubwa yenye athari, hasa kwa makampuni ya umeme ambayo yanatumia mtandao kuendeshea huduma zao."

Mara ya mwisho muangaza mkubwa kama huu ulitokea mwaka 1859.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/ZPR/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman