1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mipango ya ufadhili yatangazwa katika mkutano wa COP27

Sylvia Mwehozi
9 Novemba 2022

Suala la ufadhili limechukua hatamu katika mkutano wa COP27 nchini Misri, huku wataalamu wakichapisha orodha ya miradi yenye thamani ya dola bilioni 120 za Kimarekani kuzisaidia nchi maskini.

https://p.dw.com/p/4JHM5
UN- Weltklimakonferenz COP27 - Kanzler Olaf Scholz
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mradi wa dola bilioni 3 za Kimarekani wa kuhamisha maji baina ya Lesotho na Botswana pamoja na mpango wa kuboresha mfumo wa maji ya umma nchini Mauritius ulio na thamani ya dola milioni 10, ni miongoni mwa miradi lukuki iliyotangazwa hii leo ikijumuisha miradi 19 barani Afrika.

COP27: Mataifa makubwa yaunda muungano wa nishati ya upepoMjumbe wa Marekani kuhusu mazingira John Kerry ametangaza kuundwa kwa mfuko wa kukabiliana na gesi ya kaboni unaolenga kuyasaidia mataifa yanayoendelea kuharakisha kuondokana na matumizi ya nishati ya mafuta ya kuchimbwa. Kerry amezindua mfuko huo kwa jina la ETA kwa lengo la kufadhili miradi ya nishati mbadala na kuharakisha matumizi ya nishati safi katika nchi zinazoendelea. Chile na Nigeria ni miongoni mwa nchi ambazo zimeonyesha nia ya mapema katika mfuko huo.

"Kama hatutakuja na njia za ubunifu za kukusanya pesa tunazohitaji ili kuharakisha kipindi cha mpito katika sekta ya nishati, tutashuka chini ya nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Celsius na niko tayari kukubali kwamba tumekwama mahali ambapo hatuwezi kufikiria tofauti na kujaribu kitu tofauti ili kukamilisha kazi hii."

Ägypten | UN-Klimakonferenz 2022 in Scharm El-Scheich
Wanaharakati wa mazingira wakiandamanaPicha: Sean Gallup/Getty Images

Wakati huo huo, Afrika Kusini itapokea kitita cha euro milioni 600 kutoka Ufaransa na Ujerumani kama sehemu ya mpango wa uwekezaji wa kuisidia katika kipindi cha mpito wa nishati. Taarifa ya pamoja imeeleza kwamba "nchi hizo tatu zimesaini makubaliano ya mkopo kwa nchi mbili za Ulaya kutoa euro 300 kila mmoja ili kuisadia nchi hiyo katika juhudi zake za kupunguza utegemezi kwenye nishati ya makaa ya mawe". Afrika Kusini ambayo ni miongoni mwa mataifa 12 yenye uchafuzi duniani, inazalisha karibu asilimia 80 ya umeme wake kupitia makaa ya mawe.COP27: Viongozi kuzungumzia ongezeko la joto duniani

Katika hatua nyingine, wanaharakati wa mazingira waliandamana nje ya mkutano wa COP27 katika mji wa Sharm al-Sheikh wakipinga mabadiliko ya serikali nyingi duniani katika matumizi ya nishati ya mafuta yanayoharibu mazingira katika jitihada za kukabiliana na mzozo wa nishati. Vita vya Ukraine, miongoni mwa mambo mengine vimechangia bei za mafuta kupanda na kuchochea mataifa mengi kuzingatia tena sera zake za nishati huku baadhi zikifikiria kuvifungua viwanda vya makaa ya mawe.

Mkutano wa COP27 unafanyika wakati ulimwengu ukikabiliwa na majanga ya asili, ikiwa ni pamoja na mafuriko, joto kali na ukame uliosababisha madhara makubwa katika maeneo kadhaa duniani.