1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mimi Bado ni Binadamu - Hadithi ya Wagonjwa wa Akili Barani Afrika

12 Agosti 2013

Ulemavu ni mwiko na laana miongoni mwa watu wengi barani Afrika. Hadithi hii inaelezea jinsi familia na marafiki wa watu wenye ulemavu wanavyojaribu kuelewa na kukabiliana na hali zao. Kwani ni binadamu tu kama wengine.

https://p.dw.com/p/19MzL
Vijana wawili wanaambatana (Picha: LAIF)
Picha: LAIF

Valerie, mwanafunzi wa miaka 19 katika chuo cha uuguzi, na mwenye matarajio makubwa maishani, ameanza kusikia kelele na sauti zikivuma kichwani mwake. Hali hiyo inapozidi kuzorota anajaribu kupata matibabu bila mafanikio. Akiwa peke yake na mwenye hofu, anaanza kurandaranda mitaana ambako anadharauliwa, kutengwa na kudhalilishwa na umma usio na huruma. Je kuna mtu atakayemsaidia?

Katika sehemu nyingine ya nchi, Chumba mwenye umri wa miaka 16 anaisha katika ulimwengu uliomo kichwani mwake. Anateseka kutokana na ugonjwa wa akili na hawezi kutangamana na watu wengine wala kujitunza kama vijana wengine wa rika lake. Kwa sababu ya ugonjwa wa Chumba, majirani katika kijiji chake wanashuku mamake, Malemba, ni mchawi. Baada ya kutengwa na kutosaidiwa na watu wanaomzunguka, mama huyo jasiri anafanya kila juhudi peke yake kutafuta njia ya kumsaidia mwanawe.

Wakati huo huo, ulimwengu wa Kapaka mwenye umri wa miaka 25 unaonekana umefika mwisho. Akiwa katika ndoa changa na akitarajia kupata mtoto, Kapaka ghafla anafutwa kazi. Kutokana na wasiwasi kwamba huenda akashindwa kuitunza familia yake, anapatwa na ugonjwa wa kusononeka na kuanza kupoteza hamu yote ya kuishi.

Katika vipindi kumi vya mchezo huu wa Noa Bongo Jenga Maisha Yako, wasikilizaji wanafuatilia pandashuka za watu wanaoishi na magonjwa ya akili na kuandamana na wahusika wakuu kwenye mchezo huu katika safari yao kuelekea uponaji. Wanajifunza ugumu wa kupima na kutibu na uwezekano wa kupata matibabu. Mwishowe, wasikilizaji wanajifunza kuwa watu wenye magonjwa ya akili wana haki ya kuheshimiwa na kupendwa. Hao pia ni binadamu.

Vipindi vya Noa Bongo Jenga Maisha Yako hutayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika lugha sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.