Milipuko minne yawauwa watu 29 mjini Baghdad, Iraq
5 Januari 2012Matukio hayo yamesababisha hofu ya kuongezeka uhasama wa kikabila baada ya waziri mkuu Nuri al Maliki kutoka madhehebu ya Shia kutaka kuondolewa serikalini wanasiasa wawili wakuu wa madhehebu ya Wasunni, muda mfupi tu baada ya kuondoka vikosi vya Marekani nchini Iraq.
Kwa mujibu wa duru za polisi na madaktari, mabomu mawili yaliyotegwa ndani ya gari yaliwauwa watu 15 na kuwajeruhi wengine 32 katika wilaya ya kaskazini magharibi mwa Baghdad, Kadhimiya. Mabomu mengine mawili, moja lililotegwa kwenye pikipiki iliyokuwa imeegeshwa na jingine ambalo lilitegwa kando mwa barabara, yaliwauwa takriban watu 10 na kuwajeruhi wengine 37 katika mji uliojawa umaskini wa Sadr, kaskazini magharibi mwa Baghdad.
Polisi waliyapata mabomu mengine mawili ambayo waliyategua. Iraq ingali inakabiliwa na uasi mkubwa kutoka kwa Waislamu wa madhehebu ya Wasunni na wanamgambo wa Kishiya kwa takriban miaka tisa baada ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani ambao ulimwondoa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Saddam Hussein. Mji wa Sadr ni ngome ya mhubiri mwenye msimamo mkali wa Kishia, Moqtada al Sadr, ambaye wanamgambo wake wa Mehdi kwa wakati mmoja waliwahi kupigana na wanajeshi wa Marekani na Iraq. Sasa ni mshirika mkuu wa waziri mkuu Nuri al Maliki.
Waziri huyo mkuu aliwaghadhabishwa mahasimu wake wakati alipolitaka bunge kumwondoa serikalini naibu wake wa madhehebu ya Wasunni Saleh al Mutlaq na akataka pia kukamatwa kwa makamu wa rais wa Iraq wa Kisunni Tareq al Hashemi kwa madai kuwa anaongoza magenge ya mauaji.
Siku ya Jumatano, wabunge wa kambi ya Iraqiya inayoungwa mkono na Wasunni walisusia vikao vya bunge na baraza la mawaziri, wakilishtumu kundi la Maliki kwa kujipa mamlaka mengi ya utawala katika serikali ya muungano ambayo iliundwa kwa misingi ya kupunguza uhasama wa madhehebu.
Msururu wa milipuko ya mabomu ambayo yamewauwa watu 72 hasa katika maeneo yanayokaliwa na Washiya katika mji mkuu wa Badghad siku chache baada ya mzozo huo wa kisiasa kuanza, umeongeza hofu ya kurejea kwa ugomvi kati ya madhehebu nchini Iraq ambayo ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2006 na 2007.
Marekani na umoja wa mataifa zimeomba kuwepo utulivu wakati huu wa mgogoro wa kisiasa na kuwataka viongozi wa kitaifa kufanya mazungumzo ya kuumaliza mzozo huo, lakini hakuna mikutano ya aina hiyo iliyofanyika. Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa Martin Kobler pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu mvutano wa sasa wa kisiasa nchini humo.
Kujumuishwa kwa kambi ya Iraqiya katika serikali ya muungano kulionekana kuwa muhimu ili kuzuia kurejea kwa vurugu za kimadhehebu ambazo zilichipuka baada ya uvamizi wa Marekani mnamo mwaka 2003. Wasunni wengi walalamika kubaguliwa katika mchakato wa kisiasa tangu Saddam Hussein alipoondolewa na wengi wa Washia wakajazwa serikalini.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Josephat Charo