1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milionea ashinda uchaguzi Lesotho

11 Oktoba 2022

Chama cha mfanyabiashara tajiri aliyegeuka mwanasiasa nchini Lesotho kimeshinda uchaguzi wa bunge nchini humo lakini kikishindwa kupata wingi wa kutosha wa viti bungeni.

https://p.dw.com/p/4I1kA
Lesotho wählt inmitten einer ungelösten politischen Krise ein neues Parlament
Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Chama cha Revolutionary for Prosperity kilichoundwa miezi saba iliyopita na milionea huyo Sam Matekani kimepata ushindi wa viti 56 vya bunge la Lesotho lenye jumla ya viti 120 hii ikiwa ni kulingana na matokeo ya mwisho yaliyochapishwa na tume ya uchaguzi lakini kikikosa wingi wa kutosha ili kuumaliza mkwamo wa kisiasa wa muda mrefu katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. 

Shangwe na nderemo viliisikika kutoka mitaa mbalimbali ya mji mkuu Maseru baada ya tume kutangaza taarifa hizo zilizoashirika uthabiti wa chama hicho cha Matekane. Ikiwa ni miezi saba tu tangu kiunde chama hicho kimeonekana kuwa na mvuto wa kipekee wa umma na hasa vijana wanaotamani mabadiliko katika taifa hilo la kifalme lenye watu takriban milioni 2.1.

Lesotho | Einfluss der Staudämme auf armere Dörfer
​​​​Watu wa Lesotho wanakabiliwa na umasikini mkubwa na wanaamini mfanyabiashara huyo ataweza kuwakomboa.Picha: Roger Jardine

Hata hivyo, ushindi wa chama hicho haukuweza kufikia wingi unaotakiwa bingeni na sasa kina jukumu la kusaka uungwaji mkono. Kina upungufu wa viti vitano ili kupata wingi unaokubalika wa viti 61.

Katika kipindi chote cha kampeni Matekane alisisitiza umuhimu wa chama chake kuongoza bila ya kuungana na vyama vingine ili kutekeleza kikamilifu ajenda ya chama kuhusu maendeleo na kuwainua watu wa Lesotho wanaozingirwa na janga la umasikini, kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira na matukio makubwa ya uhalifu.

Soma Zaidi: Lesotho na Umaskini baada ya kukosa kuondolewa madeni na G8

Matekane, ni mfanyabiashara anayemiliki makampuni ya usafirishaji na ujenzi kwenye machimbo ya dhahabu ya Letseng pamoja na mikataba ya ujenzi wa barabara na mabwawa. Huko nyuma aliwahi kusema iwapo atakuwa waziri mkuu atazikabidhi biashara zake kwa mwendeshaji mwingine ili kuepusha mgongano wa kimaslahi.

Mji wangu: Maseru Lesotho

Milionea huyo anayejitanahisha kama mtetezi wa jamii ya wafanyabiashara nchini humo, alionekana kama msindikizaji tu kwenye uchaguzi. Lakini ghadhabu ya umma dhidi ya vyama vingine ilimuwezesha kupata ushindi huo, amesema mhadhiri wa siasa katika chuo kikuu cha National University of Lesotho Tlohang Letsie. Amesema watu wanamuona kama mkombozi na kwa maana hiyo atalazimika kujitia shime na kufanya majukumu yake kwa bidii ili kuwafurahisha watu waliomuamini.

Ntabiseng Morakane ni mmoja ya wanachama wake ambaye amesema "Ninafurahi bwana Sam amefanikiwa kupata kile alichokihitaji, kwa sababu alikuwa na maono kwa ajili ya Lesotho. Aliitaka kuiboresha Lesotho. Alitaka kutengeneza fursa kwa ajili ya Basotho na ninaposema fursa, ninamaanisha fursa sawa kwa kila raia wa Lesotho."

Na sasa Matekane analazimika kusaka washirika wa kuunda serikali. Anaweza kufanya makubaliano na chama cha Democratic Congress kilichoshika nafasi ya pili kikiwa na viti 26.

Vyama vingine ni Basotho Action chenye viti 6, Alliance Democrats chenye viti vinne, Movement for Economic Change ambacho pia kina viti vinne, Lesotho Congress for Democracy chenye viti vitatu, Basotho National Party chenye viti viwili na Socialist Revolutionaries chenye viti viwili.

Matokeo hayo yanaashiria anguko kubwa kwa chama tawala cha Basotho Convetion ambacho kwenye uchaguzi wa mwaka 2017, kilishinda viti 53 na kuunda serikali ya mseto.

Tizama zaidi:

Mshirika: APE