Milio ya risasi imesikika bunge la Uingereza
22 Machi 2017Polisi wa mji mkuu wa London wamesema wanalichukulia tukio la daraja la Wesminster kuwa ni la kigaidi. Watu walioshuhudia shambulio hilo la kwenye daraja wamesema waliona gari likiwavamia watu kadhaa. Huku walioshuhudia tukio la bungeni wakisema kuwa walisikia milio ya risasi.
Polisi waliojihami kwa silaha wamelizingira eneo hilo la bunge pamoja na daraja la Wesminster, na polisi wamewataka wabunge kubaki ndani ya jengo hilo. David Lidington, ambaye ni kiongozi wa bunge la Uingereza amesema hadi sasa anachoweza kuthibitisha ni kwamba kumetokea shambulio katika bunge hilo.
Aidha imeripotiwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza yupo salama baada ya kuoneka akiingia ndani ya gari iliyomuondosha katika jengo la bunge.
Mashambulio hayo yametokea katika siku ambayo Ubelgiji inatimiza mwaka mmoja tokea mashambulio kwenye uwanja wa ndege na kituo cha treni mjini Brussels yalioyosababisha vifo vya watu 32.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/rtre/afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman