Milan: Mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa umeanza:
2 Desemba 2003Mkutano wa Hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa umeanza mjini Milan, Italia kwa kutolewa miito ya kutekelezwa Itifaki ya Kyoto. Waziri wa Mazingira wa Italia, Altero Matteoli, katika hotuba yake amesema kuwa Itifaki hiyo inayolinda hali ya hewa kwa mara ya kwanza kabisa inatoa fursa ya mbinu za kimataifa za kupambana na gesi za sumu na uwezekano wa ukuaji wa kiuchumi. Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Jürgen Trittin, ameonyesha matumaini yake kuwa licha ya usemi uliotolewa hivi karibuni na Rais Vladimir Putin wa Urussi kuna uwezekano wa Itifaki hiyo kutiwa saini na Urussi baada ya uchaguzi wa Rais utakaofanywa mwezi wa Machi mwaka ujao. Baada ya Marekani kukataa kabisa kutia saini Itifaki ya Kyoto, hatima yake sasa imo mikononi mwa Urussi. Itifaki ya Kyoto inazitaka nchi zilizoendelea kiviwanda kupunguza sumu za gesi kwa wastani wa asili mia 5.2 kati ya mwaka 1990 mpaka 2012.