1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya wahamiaji Ujerumani

22 Julai 2015

Ujerumani imeshuhudia katika siku za hivi karibuni idadi kubwa ya mashambulizi ya moto yanayozilenga nyumba za kuwahifadhi wakimbizi. Jamii kote Ujerumani zimeathirika na kupanda kwa joto kuhusu suala la uhamiaji.

https://p.dw.com/p/1G2ff
Rechte Proteste gegen das Flüchtlingslager in Freital
Waandamanaji wakifanya maandamano mjini DresdenPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Wanatokea Syria, Eritrea au Kosovo, wakimbizi wanaozikimbia nchi zao mara nyingi wakiwa hawana chochote isipokuwa nguo zao tu wakitumai kupata maisha salama nchini Ujerumani.

Hadi mwezi Juni mwaka huu kiasi cha watu 179,037 waliwasilisha maombi ya kupata hifadhi nchini Ujerumani. Lakini mara kwa mara Wajerumani katika miji kadhaa nchini humu wanaweka wazi hisia zao kuwa hawawataki wahamiaji katika mitaa yao.

Na uhasama walio nao dhidi ya wahamiaji hawauudhihirishi tu katika kumbu za serikali za mitaa wakati wa mikutano au katika maandamano ya umma bali wanatumia moto.

Visa 13 vya moto Ujerumani

Mwaka huu Ujerumani imeshuhudia kiasi ya visa 13 vya mashambulizi ya moto yanayolenga makaazi yaliyotengwa kuwahifadhi wakimbizi au katika nyumba ambazo zinakaliwa na wahamiaji waliowasilisha maombi ya kupewa hifadhi. Kwa wastani mashambulizi hayo ni kama mawili kwa kila mwezi mwaka huu.

Deutschland Brand in künftiger Asylbewerberunterkunft in Remchingen bei Karlsruhe
Zimamoto wakizima nyumba iliyowaka moto mjini RemchingenPicha: picture-alliance/dpa/SDMG/Dettenmeyer

Hivi karibuni, nyumba ambayo ilikuwa tupu katika mji wa Remchingen karibu na mji wa kusini mwa Ujerumani wa Karlsruhe ilisababisha hasara ya karibu euro 70,000.

Nyumba hiyo ilikuwa itumike kuwahifadhi wahamiaji kabla ya kutiwa moto.

Alhamisi wiki iliyopita,katika jimbo jingine hali ilikuwa kama hiyo ya Remchingen,wakati huu katika mji wa Reichertshofen watu wasiojulikana waliitia moto nyumba iliyotarajiwa kuwahifadhi wakimbizi 67 mwezi Septemba mwaka huu.

Meya wa mji huo Michael Franken alishushtushwa na shambulizi hilo linalodhihirisha chuki dhidi ya wageni lakini akasimama kidete na kusema mipango ya kuwahifadhi wakimbizi hao itaendelea kama ilivyopangwa na watafanya kila namna kuhakikisha hilo linatimia ifikapo tarehe mosi mwezi Septemba kwani hawatatishwa na watu walio na uhasama dhidi ya wakimbizi.

Mashambulizi hayo sio katika eneo moja tu la Ujerumani. Katika mji ulioko mashariki wa Zossen wanaume wawili wanachama wa kundi la mrengo wa kulia lenye itikadi kali wanadaiwa kuyachoma makaazi mengine yaliyopangiwa kuwahifadhi wakimbizi. Miji mingine ambayo imeshuhudia visa hivyo ni Coesfeld, Escheburg na Hepberg.

Mengi ya mashambulizi hayo yanayalenga makaazi yanayotayarishwa kuwahifadhi wakimbizi. Baadhi ya nmumba hizo zinachomwa miezi, wiki au siku chache kabla ya wahamiaji hao kuziingia nyumba hizo.

Msemaji wa wakfu wa Amadeu Antonio Robert Lüdecke ameliambia shirika la habari la DW kuwa wanaofanya mashambulizi hayo wanataka kutoa ujumbe kuwa wanapinga kampeini ya serikali ya Ujerumani ya kuwakaribisha wahamiaji na kwa kufanya mashambulizi hayo wanatumai watawatisha wakimbizi.

Wakfu huo wa Amadeu Antonio unapambana dhidi ya itikadi kali,ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wayahudi nchini Ujerumani.

Lakini mashambulizi hayo na uhasama huo unaweza kuzuiwa vipi katika jamii ambayo inazidi kuonyesha uelewa mdogo na kuwakubali wakimbizi? Ludecke anasema maafisa wa serikali wanapaswa kuwaeleza wakaazi kwanini wakimbizi wanakuja, Wanatoroka mateso gani katika nchi zao na wanahitaji maafisa waliohitimu kupitisha ujumbe huo katika shughuli nzima ya kuwahamisisha wajerumani kuhusu utangamano na wanasiasa wanahitaji kujitokeza kwa umma kueleza sera hiyo ya kuwapa hifadhi wakimbizi.

Lakini kwa sasa, hali Ujerumani inasalia kuwa tete. Idadi ya wakimbizi wanaotafuta hifadhi haionekani kupungua hivi karibuni na ilimradi kuna wakaazi wa Ujerumani ambao bado wanawapinga wageni na wanaanzisha ramani za kuonyesha maeneo yaliyotengewa wahamiaji, kitendo cha kuchomwa kwa makaazi hayo kinaonekana kitu rahisi kufanya.

Mwandishi: CaroRobi/Dw English
Mhariri: Mohammed Khelef