Mikakati ya kuwawezesha wakimbizi kuyakidhi mahitaji yao
25 Machi 2019Katika hatua ya kushughulikia mahitaji ya zaidi ya wakimbizi milioni 3.8 walioko katika mataifa ya pembe ya Afrika, wadau husika ikiwemo Umoja Mataifa, Umoja wa Ulaya na ule wa Afrika wanalenga kutekeleza mipango ya kuwawezesha watu hao kujitegemea wenyewe.
Kwa ushirikiano na shirika la Maendeleo ya pembe ya Afrika, wadau wanaokutana Kampala wanaandaa mikakati ya kuona kwamba wakimbizi wanashiriki elimu na mafunzo ya kiufundi, biashara na kilimo ili wakidhi mahitaji yao badala ya kutegemea tu misaada kutoka kwa wahisani.
Kati ya wakimbizi milioni 6.2 duniani, milioni 3.8 kati yao wamo katika mataifa wanachama wa shirika la maendeleo pembe ya Afrika IGAD. Idadi hiyo inazidi kuongezeka kila kukicha ili hali ufadhili kwa watu hao unazidi kupungua. Ni kwa ajili hii ndipo serikali za kanda hiyo kwa ushirikiano na mashirika ya umoja mataifa umoja, benki ya dunia, mashirika ya misaada kama GIZ ya Ujerumani, asasi za kiraia pamoja na viongozi wa wakimbizi wanataka kujitokeza na mikakati ikiwemo kuwapa uwezo wakimbizi wajitegemee.
Suala nyeti hapa ni kuwezesha kuwepo kwa hali endelevu ya kuboresha maisha ya wakimbizi pamoja na jamii za wenyeji kwa kuwapa fursa za elimu, mafunzo ya stadi za kimapato na ufadhili kwao kushiriki shughuli za kipato ili wasiendelea kutegemea tu misaada lakini pia waandaliwe kurejea maisha yao ya kawaida wakirudi nchini kwao. Hilary Onek ni waziri wa majanga Uganda aliyefungua mkutano huo wa siku tatu hii leo.
Kulingana na wataalam wa Umoja Mataifa pamoja na shirika la IGAD asili mia 60 ya wakimbizi wana uwezo wa kufanya kazi za kimapato huku wale ambao ni watoto wanaweza kushiriki elimu na mafunzo yatakayowandaa kwa maisha bora.
Wakati huohuo wadau wanazingatia kuzidisha juhudi za kuwashawishi wakimbizi kurudi katika nchi zao ambako hali ya usalama na amani vimehakikishwa hivi karibuni. Wadau pia wanachunguza jinsi ya kuzisaidia jamii za wenyeji wa nchi wanaogawana raslimali zao na wakimbizi kuweza kumudu hali ya maisha bila kujenga uhasama kati yao na wakimbizi.
Aidha katika mkutano huo wa siku tatu, wadau watajadili njia za kuepusha au kukomesha mizozo ambayo ndiyo chanzo cha watu kuzikimbia nchi zao. Wakati huohuo nchi za IGAD zinataka kuhakikisha kuwa wakimbizi hawajihusishi katika masuala na harakati za kisiasa nchini kwao wakiwa ugenini kwani hii inaathiri mahusiano miongoni mwa nchi za kanda hiyo kukiwa na mashaka kama hayo.