1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miji mitano yabakia kuwania kuandaa michezo ya Olimpiki 2012

Mohamed Abdulrahman18 Mei 2004

Wakati New York, Paris, London, Madrid na Moscow ikiingia awamu ya mwisho, Leipzig, Rio, Istanbul na Havana yachujwa.

https://p.dw.com/p/CHaJ
Wakaazi wa Leipzig wakionekana wenye machonzi baada ya kuondolewa kwenye orodha ya mwisho kuwania maandalizi ya michezo ya Olimpiki 2012.
Wakaazi wa Leipzig wakionekana wenye machonzi baada ya kuondolewa kwenye orodha ya mwisho kuwania maandalizi ya michezo ya Olimpiki 2012.Picha: AP

Kinyanganyiro cha kuwania maandalizi ya michezo ya olimpiki 2012 sasa kimebakia kuwa kati ya mji wa New York na miji mikuu minne ya Ulaya baada ya miji minne mengine kuchujwa leo mjini Lusanne. -

Miji mitano iliobakia kuwania nafasi ya kuwa mwenyeji wa michezo ya olimpiki 2012 ni New York, na miji mikuu minne ya Ulaya-London, Madrid, Moscow na Paris. Ukilitenga jiji la Moscow, Paris London , Madrid na New York ikitarajiwa tokea hapo awali kuwa na uwezekano wa kubakia awamu ya mwisho ya kinyanganyiro hicho na kwa upande wa Moscow , tayari unaonekana kuwa na uzoefu wa maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya 1980.

Mji wa Paris ulitokeza usoni kabisa katika ripoti ya kamati ya Olimpiki ya kimataifa, iliotilia maanani mtazamo jumla wa kiufundi kuhusiana na maandalizi ikiwa hasa ni juu ya masuala ya miundo mbinu na usalama.

Madrid ukaibuka nafasi ya pili, ukifuatwa na London, New York na Moscow- na badae Leipzig, Rio de Janeiro, Istanbul na Havana-yote ikiwa sasa imechunjwa.

Ripoti ya kamati ya olimpiki ya kimataifa, ilisema ina matumaini ya daraja ya juu kabisa kwamba Paris, New york, London na Madrid ni miji inayoweza kuandaa michezo hiyo ya 2012 , lakini ina shaka shaka na sifa za mji wa Moscow. Ama miji mengine minne Leipzig, Rio, Istanbul na Havana imetajwa kuwa haijafikia uwezo unaohitajika kwa wakati huu.

Hali ya kijiografia, inaelemea zaidi katika kuupendelea mji wa Ulaya kuwa mwenyeji wa michezo ya 2012 baada ya ile ya msimu ya kiangazi 2008 kufanyika barani Asia katika mji mkuu wa Uchina-Beijing na ile ya msimu wa baridi 2010 kuamuliwa kuwa itafanyika Amerika kaskazini mjini Vancouver-katika mkoa wa British Columbia nchini Canada.

Kwa hivyo Paris uliokua mwenyeji wa michezo ya Olimpiki 1900 na 1924 uko nafasi ya usoni. Mji mkuu huo wa Ufaransa uliandaa kwa mafanikio mashindano ya kandanda ya kombe la dunia 1998 na yale ya riadha ya ubingwa wa dunia 2003 na wanachama wa kamati ya olimpiki ya kimataifa unauona kama unaostahiki baada ya kushindwa katika majaribio ya awali 1992 na kwa michezo ya olimpiki ya 2008.

London uliokua muandalizi wa michezo ya 1908 na 1948, unatazamwa kuwa mpinzani mkubwa katika kinyanganyiro hicho, ukiwa na baadhi ya maeneo maarufu ya michezo na sehemu za vivutio kwa utalii-ikiwa ni pamoja na uwanja wa tennis wa Wimbledon na uwanja wa Wembley ambao ukarabati wake unatazamiwa kumalizika 2006.

Madrid ni mji mkuu pekee wa Ulaya usiowahi kuandaa michezo ya Olimpik.

New York ambao haujawahi kuandaa michezo ya Olimpiki, unagubikwa na hisia dhidi ya Marekani kuhusiana na matukio ya Irak na pia inajikutakijiografia ikiwa haina nafasi kubwa kwa sababu ya Canada kuwa nchi itakayoandaa michezo ya majira ya baridi 2010. Kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki mara nyingi hujizuwia kutoa nafasi ya maandalizi kwa bara moja mfululizo.

Hakukua na mshangao kutokana na kuondolewa kwa miji mingine minne katika kinyanganyiro cha 2012. Leipzig ni mji mdogo na una uhaba wa hoteli za kutosha. Istanbul iliokua ikiwania nafasi hiyo kwa mara ya nne, haikutoa kivutio kikubwa.

Rio, ukitarajia kuwa mji wa kwanza kuandaa michezo ya Olimpik katika Amerika kusini una matatizo makubwa ya uhalifu. Na zaidi ya hayo Brazil huenda ikapewa nafasi ya kuandaa mashindano ya soka ya kombe la dunia 2014 na itakua na kazi ngumu kuandaa michezop hiyo miwili katika muda unaokaribiana. Kadhalika zingatio dogo ulipewa mji mkuu wa Cuba-Havana.

Wagombea watano waliobakia watalazimika kulipa dola 500,000 kila mmoja , kugharimia utaratibu uliobakia wa shughuli za majaji na za uteuzi.Na uamuzi wa nani atakua mwaandalizi wa michezo hiyo ya Olimpiki 2012 utatolewa Julai 20 mwaka ujao 2005, na Kikao kamili cha wajumbe wa kamati ya kimataifa ya Olimpik mjini Singapore.