Michuano ya "SportPesa Super Cup" yaanza Dar
5 Juni 2017Mashindano hayo ya mwanzo ya SportPesa Super Cup yanaungwa mkono na mashirika ya kandanda ya Kenya na Tanzania baada ya mashindano ya kanda hiyo yanayotayarishwa na shirikisho la kandanda la Afrika mashariki na kati, CECAFA kushindwa kufanyika mwaka jana.
Mashindano hayo yanaanza rasmi leo(05.06.2017) ambapo miamba ya Kenya AFC Leopards watafungua mashindano hayo kwa kuumana na Singida United ya Tanzani bara katika uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam. mabingwa wa ligi Tanzania Dar Young Africans wanapimana nguvu na Tusker ya Kenya katika mchezo wa pili leo jioni. Timu nyingine zinazoshiriki ni Simba ya Tanzania, Jang'ombe ya Zanzibar , Gor mahia na Nakuru All Stars zote kutoka Kenya.
SuperSport United ya Afrika kusini imeweza kutoka sare ya mabo 2-2 dhidi ya mabingwa wa kombe la Shirikisho , CAF Confederation Cup TP Mazembe ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo jana Jumapili. Ben Malango na Mzambia Rainford Kalaba walipachika mabao na kuwapa Mazembe uongozi wa mabao 2 , dakika 26 katika mchezo huo katika mchezo wa kundi D katika mji wa kusini nchini Congo wa Lubumbashi. Lakini Aubrey Modiba alirejesha bao la kwnza na Teboho Mokoena alisawzisha katika dakika ya 66 akiwanyamazisha mashabiki wa nyumbani.
Nayo St George ya Ethiopia iko ukingoni mwa kuingia katika awamu ya robo finali baada ya kuishinda V Club ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kwa bao 1-0. Goli la Saladin Said lilitosha kuwazamisha Vita Club , goli ambalo ni la sita kwa mshambuliaji huyo hatari , na akiwa sasa anaongoza idadi ya wafungaji mabo katika kinyang'anyiro hicho barani Afrika akifuatiwa na Msudan Bakary al Madina wa El Merrikh na Muaid Allafi wa Libya kutoka Al Ahly Tripoli wakiwa na mabao 5.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / ape / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga