1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya kombe la dunia la Soka.

Halima Nyanza21 Juni 2010

Timu ya taifa ya soka ya Brazil jana ilifanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya kombe la dunia la mpira wa miguu yanayoendelea nchini Afrika kusini, baada ya kuifunga Ivory Coast mabao 3 kwa 1.

https://p.dw.com/p/NyI7
Mchezaji wa Brazil, Luis Fabiano, akifunga bao la pili dhidi ya Ivory Coast, wakati timu hiyo zilipopambana hapo jana.Picha: AP

Brazil inakuwa timu ya pili kujihakikishia nafasi hiyo ya kusonga mbele baada ya Holand.

Katika mpambano huo wa jana usiku uliofanyika mjini Johannesburg, magoli ya Brazil yalifungwa na Luis Fabiano pamoja na Elano, wakati goli la Ivory Coast lilifungwa na Didier Drogba.

Katika mchezo huo pia, mchezaji mahiri wa Brazil, Kaka alitolewa nje baada ya kupewa kadi mbili za njano.

Na katika hatua nyingine, timu ya soka ya taifa ya Ufaransa jana iligomea mazoezi, katika kupinga uamuzi uliotolewa wa kumrudisha nyumbani mshambuliaji nyota wa timu hiyo Nicolas Anelka.

Habari zinasema uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Anelka kugombana na kocha wa timu hiyo wakati wa mapumziko katika mchezo wao na Mexico.

Uasi huo uliofanywa na timu ya taifa ya Ufaransa jana, umeelezwa kusababisha mkurugenzi wa timu Jean-Louis Valentin kujiuzulu.

Ufaransa ipo katika nafasi ngumu ya kuweza kusonga mbele katika mashindano hayo na inapaswa kushinda katika mchezo wa mwisho wa makundi, kati yake na Afrika Kusini.