1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo yacheleweshwa na mabango ya matusi

Sekione Kitojo
2 Machi 2020

Michezo ya ligi Ujerumani imeingiliwa kati na kucheleweshwa mwishoni mwa juma kutokana na mabango yenye kashfa na matusi, yakiashiria kukua kwa mpasuko kati ya shirikisho la kandanda  na mashabiki  sugu wa mchezo huo.

https://p.dw.com/p/3Yl59
Fußball Bundesliga Union Berlin vs VFL Wolfsburg Spielunterbrechung Plakat gegen Dietmar Hopp
Picha: Imago Images/Contrast/O. Behrendt

Watangazaji  wa  uwanjani  mjini Dortmund  na  Berlin walitishia  kuvunja  michezo  hiyo  hadi  pale mabango  hayo  yatakapoondolewa, wakati  mchezo  wa  Bayern Munich  dhidi  ya  wenyeji  Hoffenheim  ulimalizika  katika  hali ambayo  si  ya  kawaida  wakati  wachezaji  kutoka  pande  zote walipokuwa  wakipeana  mpira  ili  kukamilisha  dakika  10 za mwisho.

Fußball Bundesliga | Borussia Mönchengladbach - TSG Hoffenheim | Dietmar Hopp, Transparent & Fadenkreuz
Picha ya Dietmar Hopp ikionesha duara la kulengwa shabaha uwanjani lililowekwa na mashabiki wa GladbachPicha: picture-alliance/dpa/R. Weihrauch

Uingiliaji  huo  ni  ishara  pana  ya  mjadala   mkali  katika  soka  la Ujerumani  kati  ya  mashabiki  wa  vilabu  vya  kitamaduni  na  timu zile  mpya  ambazo  zimekuwa  zikipata  fedha  kutoka  kwa wawekezaji  na  wamiliki  binafsi.

Mashabiki  waliokuwa  wakionesha  upinzani  wao  walililenga shirikisho  la  kandanda   la  Ujerumani DFB  na  uamuzi  wake  wa kutoa  adhabu  ya  miaka  miwili kwa  mashabiki  wa  Borussia Dortmund  kusafiri  kwa  ajili  ya  michezo  ya  klabu  hiyo  dhidi  ya Hoffenheim, baada  ya  mashabiki  wa  Dortmund  kuweka  mabango yenye  kashfa .

Hatua  hiyo  hata  hivyo  ilisaidia  tu  kuwaamsha  mashabiki  wa timu  nyingine  kuchukua  hatua  kuhusiana  na  kile  walichosema  ni adhabu kwa  mashabiki  wote  wa  Dortmund. Mashabiki  walipata uungwaji  mkono  wa  nahodha  wa  FC Koln Jonas Hector  baada ya  ushindi  wa  timu  hiyo  siku  ya  Jumamosi  dhidi  ya  Schalke 04 , wakati  alipohoji  kwa  nini  watu 20,000 ambao  wamekuwa wakituunga  mkono  kwa  dakika  zote 90 waadhibiwe  kwa  matendo ya  wachache?

Fußball Bundesliga | 1899 Hoffenheim vs Bayern München | Dietmar Hopp und Karl-Heinz Rummenigge
Dietmar Hopp (kushoto) akiwa pamoja na Karl Heinz-Rummenigge (kulia) pamoja na wachezaji wa Bayern na HoffenheimPicha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Shutuma  nyingi  zilielekezwa  kwa  mfadhili  ya  Hoffenheim Dietmar Hopp, ambaye  amekuwa  akikosolewa   na  mashabiki  baada  ya kukwepa sheria  ya  ligi  ya  umiliki na  kuwekeza  zaidi  ya  euro milioni 350  katika  klabu  hiyo  ya  kijijini  kwake, na  kuifikisha katika  daraja  la  kwanza.

Mabango  hayo  yenye  kashfa yakimkosoa Hopp  yamepenyezwa katika  majukwaa  ya  uwanjani   katika  maeneo  mbali  mbali  ya mashabiki  katika  wiki  za  hivi  karibuni, ikiwa  ni  pamoja  na kuweka  sura  ya  Hopp, pamoja  na  kumuita  kuwa  ni  mtoto wa malaya.

Rummenigge  asikitishwa

Mwenyekiti  wa  Bayern Munich  Karl-Heinz Rummenigge  alisimama pamoja  na  Hopp  wakati  wa  mchezo  wa  Jumamosi , akitikisa kichwa  kwa  masikitiko  na  kuwaomba  mashabiki  wa   timu  yake kuliondoa  bango  hilo. Baada  ya  mchezo  huo  Rummenigge alisema  ametiwa  aibu sana  na  mashabiki  wake. "Naomba msamaha  kwake Hopp, lakini  hakuna kisingizio  cha mashabiki  hao kufanya  kile  walichokifanya."

Alipokuwa  akizungumza kuhusiana  na  mauaji  ya  chuki  ya  mjini Hanau , rais wa  shirikisho  la  kandanda  nchini  Ujerumani  Fritz Keller  amesema  kuwa  chuki  haina  nafasi  ndani  na  nje  ya uwanja.

"Katika  soka , nje  na  ndani  ya  uwanja, wakati wa  mchezo na ndani  ya  uwanja, kila  mahali  kile  kinachohusika  na  jamii, chuki na kuwatenga watu  wa  jamii  nyingine , haina  nafasi. Hii  ni  njia  ya kijinga  kabisa , ambayo  mtu  anaweza  kujivika, na  ndio  sababu hakuna  nafasi kwa  ubaguzi, hakuna  nafasi kwa  chuki  ndani  ya viwanja."

DFB-Integrationspapier Türkiyemspor Berlin
Rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani Fritz KellerPicha: DW/S. Sfregola

Fritz Keller  aliyasema  hayo  kabla  ya  matukio  ya  wiki  hii , ambayo  yameliweka kandanda  la  Ujerumani  njia  panda, wakati viongozi  wakijaribu  kuzuwia chuki , lakini  mashabiki  wakiungana kote Ujerumani   na  kuonesha  chuki  yao  dhidi  ya  mfadhili  na mmiliki wa  timu ya  daraja  la  kwanza  hapa  Ujerumani.

Chuki  haina nafasi katika  michezo

Mchezaji  wa  klabu  ya  Union Berlin raia wa  Austria Christopher Trimmel  alipoulizwa  maoni  yake  kuhusu  upinzani  wa  mashabiki kwa  hatua  ya  DFB  kuwazuwia  mashabiki  wa  Borussia  Dortmund kutosafiri kwenda  Hoffenheim, alisema 

"Mimi  pia  napendelea  sana , kujiunga  na  upinzani  wa  manbo mbali  mbali, lakini  inapokuwa  watu  wanamtukana  mtu  binafsi moja kwa  moja, hapo sikubaliani. Hiyo  hauhusiki kabisa  na  upinzani. tumewasiliana  wazi, kwamba  mabango  haya hatutaki  kuyaona."

Fußball Bundesliga | RB Leipzig vs. Bayer 04 Leverkusen
Mchezaji wa kiungo wa bayer Leverkusen Kai Havertz (kulia) akiwa pamoja na wachezaji wenzake Jonathan Tah, Karim Bellarabi na Sven BenderPicha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Pamoja  na  hayo Bayern Munich  baada  ya  kuikandika  timu  ya Dietmar Hopp, Hoffenheim  kwa  mabao 6-0 siku  ya  Jumamosi ilijiimarisha  kileleni  mwa  msimamo  wa  ligi, ambapo  timu inayofuata  ya  RB Leipzig  iliridhika  na  sare  ya  bao 1-1  dhidi  ya Bayer Leverkusen. Bayern imefungua  sasa mwanya  wa  pointi 3 dhidi  ya  Leipzig, ambayo  imejikingia  pointi 49, ikifuatiwa  na Borussia  Dortmund  yenye pointi 48.

Mchezaji  wa  kati  wa  Bayer Leverkusen Kai Havertz  baada  ya sare  dhidi  ya  Leipzig  alikuwa  na  haya  ya  kusema.

"Haukuwa  mchezo  mzuri kwetu. Ulikuwa mchezo  ovyo ovyo  na chapwaa kabisa , kutoka  kila  upande,  bila  kasi  na  hela  heka za mchezo. nafikiri , iwapo timu  moja  ingeweza  kucheza  kwa  nguvu kwa  muda wa  dakika  tano, ingeweza  kushinda. na  mwishowe  hakukuwa  na chochote  mbali  ya  pointi moja  tu."