Michezo ya Olimpiki yang'oa nanga leo Ijumaa
23 Julai 2021Michezo hiyo iliyocheleweshwa kwa mwaka mmoja kutokana na janga la virusi vya corona itafunguliwa rasmi baadaye leo na mfalme wa Japan Naruhito katika uwanja ambao hautakuwa na mashabiki wengi. Janga la corona limewalazimu waandaji wa michezo hiyo kuwapiga marufuku mashabiki katika karibu kila mchezo huku wageni mashuhuri kutoka mataifa ya nje pia wakijiweka kanda ijapokuwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe rais wa Marekani Jill Biden wakitarajiwa kuwa miongoni mwa wageni mashuhuri 950 watakaoruhusiwa kuingia uwanjani humo.
Zaidi ya wanariadha elfu 11 watashiriki katika matukio 339 yatakayofanyika katika michezo 33 tofauti katika muda wa wiki mbili zijazo lakini idadi kamili itakayoamua ufanisi ama kushindwa kwa michezo hiyo huenda ikawa maambukizo ya virusi vya corona kutokana na michezo hiyo ambayo hii leo yalifikia 106 tangu Julai 1.
Wanariadha wanaruhusiwa kufanya mazoezi na kushiriki katika mashindano iwapo watathibitishwa kutokuwa na maambukizo ya virusi hivyo licha ya kuwa karibu na mtu aliyeambukizwa lakini kwa wale watakaothibitishwa kupata maambukizo, miaka mingi ya mazoezi na bidii itakuwa imepotea bure na ndoto za maisha kuvunjika.
Katika ujumbe kupitia video aliyochapisha katika ukurasa wake wa twitter, waziri mkuu wa nchi hiyo Yoshihinde Suga amesema kuwa anawataka wanariadha hao watakaoshiriki katika mashindano mbali mbali kuonesha uwezo wao kikamilifu. Suga ameongeza kuwa wanariadha wanaoonekana kujitahidi kuwa bora zaidi duniani wanawapa motisha vijana na watoto wadogo. Lakini wanariadha mbali mbali wanaohofia maambukizo ya virusi hivyo tayari wamejitoa katika mashindano hayo huku watatu kutoka Jamhuri ya Czech wakiwa chini ya karantini baada ya kuthibitiswa kupata maabukizo ya virusi hivyo licha ya mikakati iliyowekwa ya kuzuia kuenea kwa maambukizo.