1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo ya Olimpiki ya Rio yafunguliwa

Admin.WagnerD6 Agosti 2016

Michezo ya Olympiki ya msimu wa kiangazi imeshafunguliwa rasmi mjini Rio Brazil. Sherehe hizo zilianza kwa fashifashi na ngoma na mipangilio ya dansi katika michezo ya kwanza kufanyika katika ardhi ya Amerika kusini.

https://p.dw.com/p/1JcUO
Olympia Rio 2016 Eröffnungsfeier Carlos Arthur Nuzman
Rais wa kamati ya Olimpiki ya Brazil Carlos Arthur Nuzman akizungumza wakati wa ufunguziPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Sherehe za ufunguzi wa michezo ya olimpiki mjini Rio zilianza kwa fashifashi pamoja na miondoko ya ngoma na dansi jukwaani jana Ijumaa wakati Brazil ikijaribu kusahau miaka saba ya maandalizi yaliyokumbwa na matatizo kadhaa na jamii ya wanaolimpiki wakijaribu kusahau kwa muda mzozo wa wanamichezo kutumia madawa ya kuongeza nguvu misuli yaliyopigwa marufuku yaani doping.

Olympia Rio 2016 Eröffnungsfeier Feuer
Mkimbiaji wa zamani wa mbio ndefu za marathon wa Brazil Vanderlei de Lima akiwasha moto wa OlimpikiPicha: picture alliance/dpa/L. Schulze

Wapenzi wa michezo wapatao 78,000 walijazana katika uwanja maarufu wa Maracana kuangalia tamasha hilo lililochukua muda wa saa nne ambapo wanamichezo kama Michael Phelps pamoja na wanamichezo wengine nyota wakichukua nafasi ya juu katika mashindano hayo ya kwanza ya olimpiki kufanyika katika ardhi ya America kusini.

Mwimbaji wa Brazil Paulinho da Viola aliimba wimbo wa taifa pamoja na watoto na kuanzisha tamasha hilo lililopambwa kwa taa za rangi ngoma na dansi kabla ya wanamichezo kufanya gwaride kwa kupita mbele ya watazamaji.

Olympia Rio 2016 Eröffnungsfeier Kip Keino
Rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach akimkabidhi Kipchoge Keino tuzo ya Olimpiki wakati wa ufunguziPicha: Getty Images/B. Mendes

Kuvumiliana na heshima

Watayarishaji wamesema sherehe ya ufunguzi ililenga katika kutuma ujumbe wa kuvumiliana na kuheshimiana. Lakini imekuja wakati Brazil inapambana na hali mbaya ya mdororo wa uchumi, idadi kubwa ya watu wasio na ajira na ongezeko la uhalifu pamoja na mtafaruku wa kisiasa.

Wakati muda ukikaribia wa kuanza kwa sherehe za ufunguzi, maelfu ya waandamanaji waliingia mitaani kuonesha hasira zao kwa watawala nchini Brazil na gharama za mabilioni ya dola kwa michezo hiyo.

Olympia Rio 2016 Eröffnungsfeier
Msanii akionesha uwezo wake katika wakati wa ufunguziPicha: Getty Images/J. Squire

Wakibeba mabango yanayosema "Hapana kwa Olimpiki" , kiasi ya watu 3,000 walikusanyika nje ya hoteli ya kifahari ya Copacabana Palace , ambako wanariadha wengi wanaoshiriki mashindano hayo ya olimpiki wanaishi. Polisi walikuwa tayari lakini kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu ya kutoa machozi.

Mwenge wa olimpiki

Brazil imetumia zaidi ya dola bilioni 10 kwa ajili ya miundo mbinu mipya na matayarisho kwa ajili ya michezo hiyo katika wakati wa mzozo wa kiuchumi. Sherehe hizo za ufunguzi zinaanzisha siku 17 za michezo mbali mbali ilishirikisha kundi la wanamichezo maarufu ikiwa ni pamoja na mfalme wa mbio fupi Usain Bolt na nyota katika kuogelea Michael Phelps ambayo itakamilika ifikapo Agusti 21.

Na mwenge wa Olimpiki uliingia mjini Rio kabla ya sherehe hizo, lakini gwiji wa soka la Brazil Pele alisema hataweza kuubeba mwenge huo kutokana na hali mbaya ya afya yake.

Olympia Rio 2016 Eröffnungsfeier Team Afghanistan
Timu ya Afghanistan ikipita mbele ya watazamajiPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Idadi kubwa ya wanajeshi na polisi wapatao 85,000, mara mbili kuliko ilivyokuwa katika mashindano ya Olimpiki ya mjini London mwaka 2012, watawekwa katika mji huo kuzuwia kitisho cha uhalifu wa mitaani na mashambulizi ya kigaidi.

Hali hiyo hata hivyo haijaleta unafuu , kwani kumeshanza kutokea udokozi katika kijiji cha wanamichezo wa Olimpiki.

Olympia Rio 2016 Eröffnungsfeier Team Saudi Arabien
Timu ya taifa la Saudi Arabia ikipita mbele ya watazamajiPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Ujumbe wa wanamichezo kutoka Danmark, China na Australia wameripoti tayari vifaa vyao kuibiwa. Waandishi habari wameibiwa kamera zao na laptop.

Medali 18 zitanyakuliwa katika siku ya kwanza rasmi ya michezo hiyo hii leo.

Mwandishi: Sekione Kitojo /afpe/ rtre

Mhariri: Isaac Gamba