Michezo ya makundi katika Ligi ya mabingwa Ulaya kupangwa
29 Agosti 2018Mabingwa mara tatu mfululizo ambao ndio mabingwa watetezi kwa sasa katika Champions League Real Madrid , ambao kwa sasa wanacheza bila ya Cristiano Ronaldo, mabingwa wa kombe la ligi ya Ulaya Atletico Madrid na Barcelona ni miongoni mwa timu za juu katika upangaji wa awamu ya makundi katika Champions League unaofanyika Alhamis (30.08.2018).
Chungu namba moja kinajumuisha klabu mpya ya Ronaldo Juventus , timu mbili ambazo zina nia ya kulinyakua kombe hilo kutoka mji wa Manchester pamoja na Paris Saint-Germain, Bayern Munich na Lok Moscow.
Kwa mara ya kwanza ligi za juu za Uingereza , Italia, Uhispania na Ujerumani zitakuwa na timu nne zilizomaliza nafasi za juu kutoka katika msimu uliomalizika zikiingia moja kwa moja katika awamu ya makundi, ambazo zitachezwa kuanzia Septemba 18 hadi Desemba 12.
Kama ilivyokuwa huko nyuma, timu kutoka katika ligi moja zitawekwa mbali katika upangaji huu mjini Monaco siku ya Alhamis.
Timu hizo 32 zimegawanywa katika vyungu vinne vya timu nane, ambapo chungu namba moja kitakuwa na mabingwa watetezi Real Madrid, mabingwa wa ligi ya Ulaya Atletico Madrid na mabingwa kutoka katika katika nchi sita za juu kabisa katika Ulaya.
Vyungu vingine 4
Timu nyingine 24 zimewekwa katika vyungu namba mbili hadi 4 kwa mujibu wa uwezo wa klabu, wakati Borussia Dortmund na Manchester United ni miongoni mwa timu zilizoko katika chungu namba 2, monaco na Ajax zimo katika chungu namba 3, na Galatasaray na Inter Milan ya Italia zimo katika chungu namba 4.
Makamu bingwa wa kombe la ligi ya mabingwa msimu uliopita Liverpool itakuwa katika chungu namba 2 ama 3, ikitegemea na matokeo ya michezo ya mwisho ya mechi za mchujo jioni ya Jumatano.
Ronaldo ni mfungaji bora katika Champions League katika misimu mitatu iliyopita, akiwa na mabao 120. Pia ameshinda tuzo ya goli la msimu katika bao lake la tikitaka katika ushindi wa Real wa mabao 3-0 dhidi ya Juventus, ambapo shangwe zilizotoka upande wa mashabiki wa Juventus zimemfanya amue kujiunga na mabingwa hao wa Italia.
Juve watakuwa na matumaini kwamba Ronaldo anaweza kuwasaidia kushinda taji hilo la juu katika soka la Ulaya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996, baada ya kushindwa katika fainali nne tangu wakati huo, ikiwa ni pamoja na mwaka 2015 na 2017.
Kwa upande wao Real , hivi sasa inapaswa kumtegemea Karim Benzema na Gareth Bale ambao hata hivyo wamefanikiwa kupata mabao wakati Real ilipoishinda Liverpool 3-1 kwa ubingwa mara 13 katika champions League. Pia wana kocha mpya Julen Lopetegui baada ya kuondoka Zinadine Zidane.
Pep Guardiola wa Man City na PSG, ambao sasa wana kocha mpya Thomas Tuchel raia wa Ujerumani , wanataka kunyakua kombe hilo hatimaye baada ya kufanya vibaya katika misimu iliyopita licha ya utajiri wao.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga