1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo Wikiendi: Ujerumani, Norway, nani zaidi soka ya wanawake?

27 Julai 2013

Ujerumani yasaka taji la sita mfululizo katika mashindano ya ubingwa wa soka ya Wanawake barani Ulaya. Bayern Munich na Borrusia Dortmund zapambana katika Super Cup, na Usain Bolt ashinda tena Uingereza.

https://p.dw.com/p/19FFT
Simone Laudehr (2nd l) celebrates her goal with Celia Okoyino da Mbabi, Leonie Maier and Nadine Keßler (r) of Germany during the UEFA Women's EURO 2013 quarter final soccer match between Germany and Italy at the Växjö Arena in Vaxjo, Sweden, 21 July 2013. Photo: Carmen Jaspersen/dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++
Frauen EM 2013 Deutschland ItalienPicha: picture-alliance/dpa

Fainali soka ya wanawake Ulaya
Timu ya soka ya wanawake ya Ujerumani kesho Jumapili itapambana na Norway katika fainali ya mashindano ya kombe la Ulaya mwaka 2013 kwa wanawake. Lakini ushindi huenda usiwe mwepesi sana kwa mabingwa hao mara tano wa kombe hilo la ulaya, kwa kuzingatia ukweli kwamba safari ya kufikia fainali hii haikuwa mtelemko hata kidogo. Lakini ushindi utaifanya Ujerumani kushinda taji hilo la wanawake kwa mara ya sita mfululizo. Utambuzi wa changamoto walizozipata katika michezo ya makundi utakuwa na jukumu kubwa katika kusaidia azma yao hiyo.

Timu ya wanawake ya Norway.
Timu ya wanawake ya Norway.Picha: Jonathan Nackstrand/AFP/Getty Images

Ujerumani iliipiku Iceland katika kundi B na kuingia moja kwa moja katika robo fainali kwa tofauti ya magoli. Miongoni mwa mechi zao za makundi, kilikuwemo kipigo cha goli 1-0 ilichokipata kutoka kwa Norway, matokeo ambayo yalihitimisha rekodi yao ya miaka 17 ya kutofungwa, au mechi 59 katika fainali za kombe la Ulaya kwa wanawake. Ikiwa timu ya Norway iliyohitimisha rekodi hiyo, ndiyo inakutana na Ujerumani katika fainali ya Jumapili, ni ipi nafasi ya Ujerumani kutetea ubingwa wake?

"Nadhani kila kitu kinawezekana, timu yetu imerejesha nguvu yake upya, na wachezaji wana ari na wanajitambua baada ya safari ndefu. Walifaulu kupita katika hatua ya mtoano ambayo timu nyingine kama Sweden au Ufaransa hazikufanikiwa kupita. Kwa hiyo nadhani kila kitu kinawezekana na nawatakia ushindi wa taji hilo," amesema Steffi Jones ni Mkurugenzi wa soka ya wanawake katika shirikisho la mpira wa miguu la Ujerumani DFB..

Bayern vs Borrusia Super Cup
Miamba ya soka nchini Ujerumani - Bayern Munich na Borrusia Dortmund zinapambana Jumamosi hii katika shindano la kombe la kukaribisha msimu - yaani Super Cup, katika kile kinachoonekana kama marudio ya fainali ya Bingwa wa Ulaya. Lakini klabu ya Borussia Dortmund imekanusha kuwa inataka kulipa kisasi. Ushindi wa Bayern wa magoli 2-1 dhidi ya Borrusia katika uwanja wa Wembley mjini London mwezi Mei ulimaanisha kuwa Bayern ilikuwa timu ya kwanza ya Ujerumani kushinda mataji matatu katika msimu mmoja, lakini Borussia Dortmund wanaiona mechi ya leo kama kipimo kuliko kulipa kisasi cha Wembley.

Mlinzi wa Borussia Dortmund Mats Hummels amesema hiki siyo kisasi cha Wembley ni kipimo kwa wao kujua wanasimama wapi, na wala hawataweka hamasa yao juu ya ukweli kwamba walishindwa mjini London. Klabu hizo mbili zimeshinda mataji manne yaliyopita ya Bundesliga kati yao na bila shaka kuna msisimko mkubwa kimataifa katika mechi hii, ambayo inaonyeshwa katika mataifa 195. Wakati BVB hawataanza na wachezi wao watatu wapya, Bayern inatizamiwa kuwa na kikosi chake kamili.

Beyern Munich ikichuana na Borrusia Dortmund.
Beyern Munich ikichuana na Borrusia Dortmund.Picha: Augenblick

Uwanja wa kifo Hong Kong
Kocha wa Machester United David Moyes amekiri kuwa na wasiwasi juu ya uwanja wa mjini Hong Kong, ambako timu yake ilifikia katika duru ya mwisho ya ziara yao ya bara la Asia. Mabingwa hao wa Ligi kuu ya Uingereza wanacheza na wenyeji klabu ya Kitchee siku ya Jumatatu katika uwanja wa Hong kong wenye uwezo wa kupokea watazamaji elfu 40,000, ambao hata hivyo unaelezwa kuwa umeathiriwa vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha kwa muda mrefu.

Meneja wa klabu ya Sunderland Paolo Di Canio, aliuita uwanja huo siku ya Ijumaa kuwa wa 'mauaji' wakati bosi ya klabu ya Tottenham Hotspurs Andre Villas-Boas alishuhudia mlinzi wake Jan Vertonghen akiondolewa kwenye machela baada ya kuumia kifundo cha mguu akicheza katika uwanja huo. Mvua zaidi ilinyesha mjini Hong Kong baada ya Manchester kuwasili, na ilitarajiwa kuendelea kunyesha siku za Jumapili na Jumatatu.

Fabregas hauzwi kwa dau lolote
Naye kocha mpya wa klabu ya Barcelona Gerardo Martino amebainisha wazi kuwa mchezaji wa kiungo Cesc Fabregas hatouzwa kwa klabu ya Manchester United au klabu yeyote nyingine. United imekwishaisogelea mara mbili Barcelona na bei tofauti kwa ajili ya Fabgegas, na mara zote mabingwa hao wa Uhispania waliitolea nje, ikiwemo ya dola za Marekani milioni 38. Mabingwa hao wa Uingereza sasa wameripotiwa kupandisha dau lao. Fabregas bado yuko na timu yake mjini Oslo kwa mechi za kirafiki za maandalizi ya msimu na kocha huyo mpya alitarajiwa kuungana nao leo. Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari, Kocha Martino amewahakikishia mashabiki kuwa Fabregas hatouzwa kwa dau lolote lile.

Wakati huo huo, kocha wa klabu ya Chelsea Jose Mourinho amesema hana wasiwasi kuhusiana na mpango wake wa kumtaka mchezaji wa Manchester United Wayne Rooney, baada ya nyota wake chipukizi Romelu Lukaku kung'arisha sifa yake inayozidi kukua kwa magoli mawili mjini Jakarta. Mourinho alisema hakukuwa na pendekezo jipya kwa Rooney baada ya United kukataa lile la awali, lakini pia alisema kuwa Chelsea inasimama na uamuzi wake wa kutowalenga wachezaji wengine.

Cesc Fabregas.
Cesc Fabregas.Picha: Reuters

Kocha huyo Mreno ameweka matumaini yake kwa Wayne Rooney, na Chelsea haitizamii kununua mchezaji mwingine baada ya kuwasajili mshambuliaji wa Ujerumani, Andre Schurrle mwenye umri wa miaka 22, kiungo wa kati wa Uholanzi, Marco van Ginkel mwenye umri wa miaka 20, na mlinda mlango mkongwe wa Austaralia, Mark Schwarzer mwenye umri wa miaka 40. Lukaku ambae alifunga goli la ushindi kwa mkwaju wa penati mjini Bangkok na aling'ara pia mjini Kuala Lumpur, alifunga magoli mawili siku ya Alhamisi na kuendeleza juhudi zake za kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza msimu ujao.

Chelsea ilishinda taji la lingi kuu ya Uingereza mara mbili chini ya Mourinho, na sasa wanatizamwa kama tishio kwa mabingwa wa sasa Manchester United, na washindi wa mwaka 2012 Manchester City, ambazo zote zina makocha wapya.

Mashindano ya Formula One
Mashindano ya magari ya Formula One leo yamepiga hatua kuelekea kusaini mkataba mpya wa kibishara wa miaka saba, ambao ni muhimu kwa mustakabali wake, baada ya wamiliki wa haki za mashindano hayo na shirika linaloongoza mashindano ya mbio za magari duniani FIA, kusema kuwa wamesaini nyaraka za kwanza kuelekea katika hatua za mwisho.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na kundi la Formula One na FIA katika mashindano ya Grand Prix ya Hungary, imesema kundi la Formula One na FIA wamesaini makubaliano yanayounda mfumo wa utekelezaji wa mkataba wa Concorde wa mwaka 2013, ambao utekelezaji wake utaanza baada ya kupata idhini ya vyombo vyote vya uongozi katika wiki zijazo. Mkataba wa Concorde, ambao muda wake uliisha mwaka uliopita, unashughulikia upande wa kibiashara wa mchezo huo wenye fedha nyingi, ikiwemo mgawanyo wa mapato.

Sebastian Vettel, dereva wa Red Bull katika Formula One.
Sebastian Vettel, dereva wa Red Bull katika Formula One.Picha: Getty Images

Bernie Ecclestone, bilionea wa Uingereza mwenye umri wa miaka 82, ambae anaiendesha Formula One kwa niaba ya kampuni ya CVC amezungumzia kuisajili katika soko la hisa la Singapore mwishoni mwa mwaka huu. Na baada ya mapunziko ya wiki tatu, mashindano hayo ya Formula one yanaanza tena wikendi hii ambapo timu ya Red Bull inatizamia kufuzu katika mashindano ya Grand Prix ya Hungary, Jioni ya leo.

Usain Bolt ashinda Uingereza
Bingwa mara sita wa mbio za Olimpiki Usain Bolt ameshinda mbio za mita 100 katika sekunde 9 na micro sekunde 85, baada ya kurejea katika uwanja wa Olimpiki kushiriki michezo ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kumalizika kwa mashindano ya London. Bolt aliwashinda Mmarekani Michael Rodgers alieshika nafasi ya pili na Mjamaika mwenzake Nesta Carter alieshika nafasi tatu kwa kutumia sekunde 9 na micro sekunde 99. Bolton ambaye anatizamia kurejesha ubingwa wa dunia mjini Moscow mwezi ujao, alisema ni jambo la furaha kushindana mjini London, lakini mwanariadha huyo anaeshikilia rekodi ya dunia alikiri kuwa anahitaji kufanya kazi ya ziada kabla ya mashindano ya mwezi ujao.

Usain Bolt
Usain BoltPicha: AFP/Getty Images

Manny Pacquiao kurudi ulingoni
Katika masumbwi, bondia maarufu nchini Ufilipino Manny Pacquiao ametabiri pambano la kukata na shoka kati yake na Mmarekani Brandon Rios Novemba 24, wakati akitizamia kuanza kushinda tena mataji na kuwanyamanzisha wanaozungumzia kustaafu kwake baada ya vipigo viwili mfululizo. Hii itakuwa mara ya kwanza ulingoni kwa Pacquiao ambae ameshinda mapambano 54, kutoka sare mara tano na kushindwa mara mbili, baada ya knock out mbaya aliyopigwa na hasimu wake wa muda mrefu Juan Manuel Marquez mjini Las Vegas mwezi Disemba, kipigo ambacho wengi walitabiri kingeashiria mwisho wa bondia huyo mwenye umri wa miaka 34.

Lakini amepanga shindano lisilo la ubingwa na Rios ambae pia aliambulia kipigo cha pointi dhidi ya Mike Alvarado katika uzito wa kati mjini Las Vegas mwezi Machi. Lakini Rios mwenye umri wa miaka 27, mwenye rekodi ya kushinda mara 31 na sare moja na kipigo kimoja, alisema ana uhakika wa kupata ushindi dhidi ya Pacquiao na kurejea katika mashindano ya ubingwa.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe,DW
Mhariri: Daniel Gakuba