Miaka sita baada ya uvamizi wa Iraq
20 Machi 2009Kwa mujibu wa Chama cha Kimataifa cha Msalaba Mwekundu, hali ya kiutu katika sehemu nyingi ni mbaya. Inatathminiwa kuwa kama Wairaki milioni 4.4 walioikimbia nchi yao au kuhamia sehemu zingine nchini humo humo,wanaendelea kuteseka huku Marekani iliyohusika kwa sehemu kubwa na mzozo huo,ikisita kukabiliana na matokeo ya uvamizi wake. Kwa maoni ya profesa wa Kimarekani, Michele Pistone, mzozo wa wakimbizi wa Kiiraki ni msiba mkubwa wa kiutu. Wakimbizi wengi wanasema kuwa wamekumbana na matatizo ya kubakwa na kuteswa na wengine wameshuhudia familia au marafiki wakitekwa nyara au wakiuawa. Kama Wairaki milioni 2 wamekimbilia nchi jirani hasa Syria na Jordan ili kujiepusha na vita vya Irak.
Jordan yenyewe,inakabiliana na matatizo ya ukosefu wa ajira uliofikia takriban asilimia 13. Balozi wa Jordan mjini Washington, Mwanamfalme Zeid Raad Zeid, amesema Jordan imetumia dola bilioni 1.4 kuwahudumia wakimbizi wa Kiiraki.
Lakini huko Marekani wakimbizi wa Kiiraki mara nyingi hawasaidiwi kuanzisha maisha mapya. Kwa mfano, mkimbizi Saad, aliekataa kutaja jina kamili amesema kuwa yeye alikwenda Marekani mwezi wa Mei mwaka jana akiwa miongoni mwa Wairaki waliohatarisha maisha yao na ya familia zao.Yeye alipewa viza maalum kwenda Marekani baada ya kuwafanyia kazi Wamarekani kama mkalimani kwa muda wa miaka minne. Wanawe wawili wangali huko Irak. Ameambiwa hawatoweza kwenda Marekani kwa sababu wameshapindukia umri wa miaka 21. Lakini Profesa Pistone anasema kuwa Marekani lazima ijitahidi zaidi kusuluhisha mzozo huo kwani kwa sehemu kubwa ndio iliyosababisha hali hiyo.
Kwa upande mwingine, hata huko Irak hali ya usalama bado haijaimarika licha ya kuwepo maendeleo fulani katika maeneo mengi. Katika mwaka 2007 zaidi ya Wairaki 17,000 waliuawa katika mashambulio yaliyofanywa nchini Irak. Mwaka 2008 idadi ya vifo ilikuwa 6,772 na katika kipindi cha miezi miwili ya kwanza mwaka huu wa 2009 kumetokea vifo 449, hiyo ikiwa ni idadi ndogo kabisa tangu uvamizi wa Machi 20 mwaka 2003.
Hata hivyo hali ya kiutu katika sehemu nyingi nchini humo ingali mbaya, licha ya serikali kujitahidi kuwapatia wananchi maji na huduma za afya. Bado kuna kazi nyingi za kufanywa ili kuhakikisha kuwa Wairaki wanakidhiwa mahitaji yao ya kimsingi.Vikosi vya Marekani vinatazamiwa kuondoka kutoka miji ya Irak ifikapo mwisho wa mwezi wa Juni na majeshi yote yataondoka Irak mwaka 2011.
Mwandishi: P.Martin/AFPE
Mhariri: O.Miraji