Miaka mitatu na Bin Laden bado hajakamatwa
8 Septemba 2004Mkuu wa shughuli za kukabiliana na ugaidi katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani Joseph Cofer Black, alisisitiza hivi majuzi kuwa walikuwa wanakaribia kumakamata Osama Bin Laden. Lakini maafisa wa Pakistan wamesema hawana matumaini ya kumkamata. Waziri wa habari nchini Pakistan, SHEIKH RASHID; amesema kuwa hana habari yoyote kuhusu Bin laden ingawa watu wengi wamekamatwa.
Waziri wa mambo ya ndani nchini humo,AFTAB AHMED SHERPAO, alisema ni mapema sana kwa serikali kusema kwamba inakaribia kumkamata Bin Laden.
Tangu kuondolewa mamlakani kwa mfumo wa Taliban nchini Afghanistan, kwa kumficha Osama Bin Laden, Marekani imekuwa na zaidi ya wanajeshi elfu kumi katika wakati mmoja wakimsaka Osama Bin Laden.
Zawwadi ya dola milioni 25 imewekwa kwa yeyote atakayetoa habari itakayoongoza wapelelezi kumkamata kiongozi huyo wa kundi la Al-Qaeda. Wapelelezi wanabahatisha tu kuhusu mahala anaweza kuwa lakini hawajui mahala hapo ni wapi.
Mchambuzi wa kijeshi nchini Pakistan, Talat Masood, amesema kuwa matumaini ya kumkamata Bin Laden hapo awali yalikuwa juu kuliko yalivyo sasa. Aliongeza kuwa itawabidi wapelelezi kuanza upya upelelezi huo ili kupata njia mpya za kumfikia Bin Laden, kwani njia ambazo wamekuwa wakizitumia hazina uwezekano wa kuzaa matunda hivi karibuni.
Fikira zote kuhusu mahala yuko Bin Laden, zinalenga hasa mpaka kati ya Afghanistan na Pakistan ambao una urefu wa kilomita 2,500. Mpaka huo unapita sehemu iliyojitenga, ambako hali za kuishi ni ngumu na kunatawaliwa na kabila la Pashtun. Wapashtun ni wapinzani wakuu wa Marekani na wanaunga mkono wapiganaji wa kiislamu ambao wanavamia Marekani.
Mara ya mwisho kulipokuwa na habari yoyote kumhusu, ilisemekana kuwa yuko katika milima ya Tora Bora karibu na mpaka wa kusini mashariki na Pakistan mnamo Desemba mwaka wa 2001.
Mahala hapa ndipo majeshi ya Marekani yalifanya mashambulizi ya mwisho dhidi ya wapiganaji wa Taliba.
Maelfu ya wapiganaji wa Taliban na Al-Qaeda walitoroka vita vilipokoma,wengi wao wakiingia katika milima nchini Pakistan, sehemu ambazo zinatawaliwa na makabila.
Tangu wakati huo Bin Laden amekuwa ni sauti tu katika kanda za video ambazo hazionyeshi zilirekodiwa lini.
Kanda hizo za video huwa zinajitokeza mara kwa mara kupitia watu wasiojulikana, ambao wanawapatia waandashi wa habari wa vituo vya televisheni vya Arabia.Wakati mwingine kanda hizo zinachezwa katika simu hadi katika vituo vya televisheni vya Kiarabu.
Ingawa mashirika ya upelelezi ya kimataifa yanasema sauti hiyo ni ya Osama Bin Laden, hakuna njia ya kuhakikisha kama sauti hiyo ilrekodiwa kabla au baada ya yeye kupotea.
Bin Laden anaifahamu vizuri Afghanistan na kaskazini magharibi mwa Pakistan. Mnamo mwaka wa 1984, Bin Laden ambaye anatoka familia tajiri nchini Saudi Arabia, aligharamia na kuongoza kikosi cha wapiganaji elfu ishirini wa kiislamu dhidi ya wanajeshi wa Muungano wa Soviet uliokuwa unatawala Afghanistan.
Tangu wakati kulipokuwa na fununu kwamba yuko Tora Bora, habari zingine zinasema kuwa yuko katika pango moja katika milima ya Hindu Kush. Sehemu zingine ambazo pia zimetajwa kama makazi ya gaidi huyo ni katika mikoa ya kusini na kaskazini ya Waziristan, katika eneo linalojulikana kama Devils Triangle ambako Afghanistan, Pakistan na Iran zinakutana.
Mkuu wa Upelelezi wa mkoa wa Pakistan wa Kandahar, Abdullah LAGHMANAI anadai kuwa Bin Laden alionekana katika eneo la Bajaur linalotawaliwa na makabila.
Mchambuzi wa Al-Qaeda, Peter Bergen, anafikiri Bin Laden yuko katika moja kati ya miji mingi yenye idadi kubwa ya watu nchini Pakistan, ambako watatu kati ya malieutenant wa Osama Bin Laden walikamatwa.
Uwezekano mwingine ni kwamba Bin Laden yuko katika milima ya Kashmir nchini Pakistan, eneo ambalo haliendeki na watu kutoka nje. Sehemu hiyo pia ni makazi ya wapiganaji wa Kashmir, wengi wao wakiwa na uhusiano mkubwa na Al-Qaeda.
Mchambuzi wa Pakistan, Masood anaamini kuwa Bin Laden ambaye ana urefu wa nchi sita na futi sita, na ambaye amezingirwa na walinzi wake, huenda yuko katika maeneo ambayo hawezi kupatikana, nchini Afghanistan, ambako maeneo ya mashambani hayatawaliwi na serikali kuu.
Alizidi kueleza kuwa kuwepo kwa wanajeshi wapatao laki moja katika eneo la kaskazini magharibi mwa Pakistan, ambalo ni eneo la utawala wa makabila, kunatoa uwezekano wowote wa mtu kujificha huko bila ya kupatikana.
Masood aliongeza kuwa urefu wa Bin Laden pamoja na walinzi wake unamfanya Bin Laden kutambulika haraka, na hivyo hakuna uwezekano kuwa yuko katika miji ya Pakistan au hata vijijini, kwani watu wa vijijini wanamtambua mgeni mara moja.
Masood anamaliza kwa kusema kuwa Bina Laden lazima yuko nchini Afghanistan ,hasa kusini au kusini mashariki, mahala ambapo sheria ya utawala wa serikali haufiki.
Lakini maafisa wana matumaini kuwa ingawa hakuna habari yoyote kuhusu mahala Bin Laden yuko, wanasisitiza kuwa sasa wana habari kuhusu kule alipokuwa anajificha.