1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka mitano, bado vita vyaitikisa Yemen

8 Julai 2019

Vita vya Yemen vimeingia miaka mitano leo 08.07.2019 tangu vilipoanza mwaka 2014 baada ya waasi wakihouthi wanaoungwa mkono na Iran kuuteka mji mkuu Sanaa na kuudhibiti kikamilifu

https://p.dw.com/p/3Lk4R

Jemens Houthi-Bewegungstruppen sind beim Rückzug aus dem Hafen Saleef in der Provinz Hodeidah zu sehen
Picha: Reuters/A. Zeyad

Vita katika nchi hiyo masikini kabisa katika ulimwengu wa kiarabu vilianza baada ya kundi  la waasi la Houthi lililoipindua serikali ya rais Abed Rabbo Mansouri Hadi  kuuteka mji mkuu Sanaa.Toka wakati huo mapambano yamekuwa yakiendelea ambapo baadae ilishuhudiwa vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Saudi Arabia vikishirikiano na serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa vikaingilia kati na kupambana na waasi hao wakihouthi tangu mwaka 2015. 

Mashambulizi yanayoongozwa na Saudia Arabia yamekuwa yakilenga shule,mahospitali na hata sherehe za harusi wakati waasi wakihouthi wakitumia ndege zisizokuwa na rubani pamoja na makombora kuishambulia Saudi Arabia na wamekuwa wakizilenga meli katika bahari ya Shamu.

Raia wa Yemen wameshuhudia mengi yakutia uchungu katika mgogoro huu uliowauwa maelfu ya watu na kusababisha mgogoro mbaya kabisa  wa kibinadamu ambao haujawahi kuonekana duniani na kuitumbukiza nchi hiyo katika hali mbaya ya njaa.Saeeda ambae hakutowa jina lake la pili ni miongoni mwa raia walioacha bila makazi nchi humo anasikitishwa na hali ilivyo.

''Ikiwa msaada wa kibinadamu utasitishwa,tutakuwa katika hali mbaya sana.Itakuwa baa la njaa.Watoto hawatopata chakula na watu watakufa.Mashirika ya msaada wa kiutu ndio yanayotufadhili katika yote hayo''

Ramadan Islam Religion
Picha: Reuters/K. Abdullah

Hali ya mateso kwa watoto nchini Yemen imetajwa na Umoja wa Mataifa kuzidi  kuwa mbaya. Mpaka wakati huu mapigano yanaendelea katika nchi hiyo ambapo jana tu kiasi wanajeshi 10 wa vikosi vya serikali katika mji wa Hodeida waliuwawa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na waasi. Mapigano yalichacha wiki iliyopita siku ya Jumatano ambapo raia saba walijeruhiwa baada ya kombora kulenga makaazi ya watu katika mji huo ulioko kwenye eneo la bahari ya shamu.

Serikali inayotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa imewashutumu waasi kwa kutumia majengo ya Umoja wa Mataifa katika mji wa Hodeida kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake.

Mashambulizi hayo ya karibuni yametokea ikiwa ni miezi miwili baada ya waasi wakihouthi kudai kujiondowa kutoka mji huo wa bandari wa Hodeida hatua ambayo serikali iliikosoa kwa kusema ni kiini macho.

Lakini kwa upande mwingine vikosi vya muungano vikiongozwa na Saudi Arabia katika vita hivyo viliripoti siku ya Jumamosi kwamba wanajeshi wake wameizuia ndege isiyokuwa na rubani iliyokuwa imerushwa na waasi hao wakihouthi kutokea mji mkuu Sanaa  kuelekea nchini Saudia,ingawa waasi wakihouthi wameyakanusha madai ya Saudi kwa kusema ndege hiyo ilifanikiwa kushambulia na kusababisha kufutwa kwa safari za ndege katika viwanja viwili vya Saudi karibu na eneo la mpaka na Yemen upande wa Kusini.

 Kituo kinachorusha habari kwa njia ya  setalaiti cha Wahouthi cha Al Masira kilitangaza kwamba waasi hao walivishambulia viwanja vya ndege vya Abha na Jizan  kwa ndege zisiziokuwa na rubani za Qaef 2K.Wahouthi wamesema wametengeneza silaha za kisasa kabisa ambazo watazitumia kupambana na vikosi vya muungano.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW