Libya bila ya Gaddafi
20 Oktoba 2016Eti kulikuwa na umuhimu wa kuunga mkono mapinduzi ya Libya na kukomesha utawala wa kimabavu wa kanali Muammar Gaddafi?Miaka mkitano baadae,Libya imezama katika bahari ya vurugu na masuala kuhusu umuhimu wa kuingilia kati wakati ule yazidi kuhanikiza.
Mwezi Machi mwaka 2011,viongozi wa magharibi,wakitanguliwa na rais wa wakati ule wa Ufaransa Nicolas Sarkozy hawakuwa na shaka yoyote kwamba ;Mapinduzi ya Libya yaliyoanza Februari baada ya vuguvu la kiangazi nchini Tunisia, yalihatarishwa na Gaddafi .
Lakini ikiwa kujiingiza nchi za magharibi kumezuwia balaa la mauwaji,uamuzi huo umepelekea pia kuporomoka utawala wa miaka 42 wa Gaddafi aliyeuliwa kinyama kabisa Oktoba 30 ya mwaka huo huo kwa hujuma za mabomu ya jumuia ya kujihami ya NATO.
"Hamkudhamini majukumu ya baadae" Lawama hizo rais Idriss Deby wa Chad alizItoa wakati ule,mpaka leo zina uzito.Licha ya uchaguzi mwaka 2012 ambao waliberali waliibuka na ushindi,Libya imezama katika bahari ya vurugu na kuishi katika vitisho vya makundi ya wanamgambo.
"Jumuia ya kimataifa ilibidi iwe imeandaa mkakati wa siku zitakazofuatia kung'olewa madarakani Gaddafi" analalamika Mahmud Djibril,kiongozi wa zamani wa baraza la mpito la taifa-taasi ya waasi iliyotambuliwa mwaka 2011 na nchi za magharibi.
Juhudi kadhaa za kimataifa zinaendeshwa kusaka ufumbuzi wa mzozo wa Libya, amesema Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Martin Kobler, wakati akizungumza na DW.
"Nnaamini moja kwa moja kwamba mzozo wa Libya unabidi upatiwe ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo na sio kwa njia za kijeshi.Na hilo ndilo nnalo lipigania mie. Na sitochoka kuzitanabahisha paande zote nchini Libya,Mashariki,magharibi na Kusini kwamba mazungumzo ndio njia pekee ya kuufumbua mzozo wao.Pale ambapo sisi tunaweza kusaidia,tutasaidia,na bila ya kuingilia kati.
Martin Kobler anapanga kuonana wiki inayokuja na rais wa zamani wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambae ndie mwaakilishi mkuu wa umoja wa Afrika kuhusu Libya. Atakutana pia na katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu ili kwa pamoja waweze kuzungumzia namna ya kuisaidia Libya.
Walipopigania kutimuliwa madarakani Gaddafi, miaka mitano iliyopita walibya walitegemea wangekuwa na mustakbal mwema. Hii leo, matarajio yao yamepwaya; "Kuishi salama,kuwa na aumeme,mafuta,mshahara na kuwapeleka watoto wetu shule. Hatutaki zaidi" aynaasimulia Mahmoud, mkaazi wa Tripoli mwenye umri wa miaka 35.
Kila asubuhi mikururo ya watu wanapiga foleni mbele ya benki ambazo hazina uwezo wakupata fedha taslimu kukidhi mahitaji ya wateja wake.
Sambaamba na hayo walibya wanakumbwa na ughali wa bidhaa ambao haujawahi kushuhudiwa.Bei za vyakula zimepanda kwa asili mia 31 mnamo nusu ya kwanza ya mwaka-hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya benki kuu ya dunia.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFPE/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel