Miaka minne tokea kifo cha Yasser Arafat kiongozi wa Wapalestina.
11 Novemba 2008Hata hivyo hakuna matukio yoyote yale yaliopangwa kwa kumbukumbu hiyo katika Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema wakati unayoyoma kuweza kufikiwa amani ya Mashariki ya Kati kwa ufumbuzi wa kuwepo kwa mataifa mawili la Israel na la Wapalestina.
Mohamed Dahman na taarifa kamili.
________________________________________
Kamati ya maandalizi imeshutumu kundi la Hamas kwa kukwamisha juhudi zake za kuandaa matukio yoyote yale ya kumbukumbu ya kifo hicho cha Arafat katika eneo hilo la mwambao ambalo kundi hilo la siasa kali za Kiislam lilichukuwa kwa nguvu kutoka kwa vikosi vilivyo tiifu kwa kundi la Fatah la Arafat lisilo la kidini hapo mwezi wa Juni mwaka jana.
Mrithi wa Arafat kama kiongozi wa Fatah na Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas alikuwa anatazamiwa kuhutubia katika makao makuu yake ya kisiasa kwenye mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah ambapo ndiko alikozikwa Arafat.
Wapalestina kutoka miji yote ya Ukingo wa Magharibi wamesafiri kwenda Ramallah kwa ajili ya kumbukumbu hizo wakipeperusha bendera za taifa na maberamu ya Fatah.
Kumbumkubu hizo zilikuwa zionyeshwe kwenye televisheni ya Wapalestina ambayo imekuwa ikipiga nyimbo za kumtukuza Arafat kutwa nzima ya leo.
Mwaka jana maandamano makubwa ya kumbukumbu ya kifo cha Arafat huko Gaza yaliingia dosari kutokana na ghasia baada ya polisi wa Hamas kuufyetuwa risasi umma na kuuwa watu wanane na kujeruhi wengine 130.
Arafat alikufa katika hospitali ya Ufaransa hapo tarehe 11 mwezi wa Novemba mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 74.
Sababu halisi ya kifo chake bado haijulikani lakini viongozi kadhaa wa Wapalestina wamedai kwamba alipewa sumu na Israel ambayo imekanusha vikali madai hayo.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert kwa mara nyengine ametetea kufikia makubaliano ya amani ambayo kwayo Israel itajitowa takriban katika eneo zima la Ukingo wa Magharibi inalolikalia kwa mabavu.
Akizungumza katika kumbukumbu ya kifo cha Yitzhak Rabin waziri mkuu wa Israel aliyeuwawa na Myahudi wa siasa kali za kizalendo hapo mwaka 1995 muda wa kupata uvumbuzi wa mzozo wa Mashariki ya Kati kwa kuanzishwa kwa taifa huru la Wapalestina pembezoni mwa Israel unayoyoma na kwamba uamuzi lazima uchukuliwe hivi sasa bila ya kusita kabla ya fursa hiyo ndogo iliopo kuweka ufumbuzi huo mawazoni mwa watu wao na mataifa duniani kutoweka mbele ya macho yao.
Pia katika hotuba yake kwa bunge hapo jana katika kumbukumbu ya kifo cha Rabin Olmert amesema Israel inatakiwa kuachilia sehemu kubwa ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na Jerusalem ya mashariki na Milima ya Golan ya Syria kwa kubadilishana na amani.
Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni leo amejitenganisha na matamshi hayo ya Olmert ya kubadilishana ardhi kwa amani na Wapalestina.
Katika mahojiano na radio ya kijeshi Livni ambaye atakiongoza chama cha mrengo wa wastani cha Olmert cha Kadima katika uhaguzi wa mwezi wa Februari mwakani amesema habanwi na sera za waziri mkuu huyo anayeondoka madarakani.
Amesena anabanwa na sera za chama chake cha Kadima ambazo amezirasimu na ambazo kwayo zimeweka misingi ya majadiliano na Wapalestina ambayo dunia nzima inaweza kuunga mkono.