1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 90 ya kuzaliwa Malkia Elizabeth II

Admin.WagnerD21 Aprili 2016

Malkia Elizabeth wa Uingereza amesherehekea mwaka wake wa 90 wa kuzaliwa Alhamisi (21.04.2016), na kudhihirisha dhamira yake ya kuendelea kufanya kazi aliyoianza miongo sita iliyopita.

https://p.dw.com/p/1IaSr
Malkia Elizabeth akiwa kwenye gari la wazi na mume wake Mwanamfalme Philip.
Malkia Elizabeth akiwa kwenye gari la wazi na mume wake Mwanamfalme Philip.Picha: picture alliance/empics/J. Stillwell

Kawaida siku ya kuzaliwa ya Malkia hupita bila sherehe zozote lakini katika kuadhimisha tukio hilo muhimu la kihitoria siku ya leo, Elizabeth aliekuwa amevalia nguo ya rangi ya kijani, alichanganyika na makundi ya watu wakati wa matembezi marefu karibu na kasri lake la Winsdor magharibi mwa London.

Na baadae katika hatua ya nadra katika miaka ya karibuni, aliendeshwa kuuzunguza mji wa Windsor katika gari la wazi akiwa sambamba na Mwanamfalme Philip, mume wake kwa miaka 68. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amemtaja Malkia Elizabeth kama mwamba wa uimara wa taifa hilo, katika ujumbe wake wa kumtakia kheri katika maadhimisho ya miaka 90 ya kuzaliwa kwake.

"Katika zama hizi za kisasa za Elizabeth ambamo mambo mengi yanayotuzunguka yamebadilika, Malkia ameendelea kuwa mwamba wa uimara wa taifa letu, wa jumuiya ya madola na katika matukio mengi kwa dunia nzima. Ndiye malkia wetu na hivyo tunajivunia sana. Heri ya siku ya kuzaliwa Malkia wetu, na tunakuombea maisha marefu na uendelee kutuongoza sote," alisema waziri mkuu Cameron.

Malkia Elizabeth akipokea maua kutoka kwa watu waliojitokeza kujumuika naye katika maazimisho ya siku yake ya kuzaliwa.
Malkia Elizabeth akipokea maua kutoka kwa watu waliojitokeza kujumuika naye katika maazimisho ya siku yake ya kuzaliwa.Picha: Reuters/S. Wermuth

Wasaidizi wa karibu wanasema Elizabeth ambaye amekalia kiti cha Umalkia kwa miaka 64 sasa, na akiwa ndiye aliekikalia kiti hicho kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Uingereza, alipendelea zaidi matukio kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, kuliko kuhusu kumpiku bibi yake mzaa bibi Malkia Victoria Septemba mwaka jana kama mtawala wa muda mrefu zaidi wa Uingereza.

Raia wamtaka aendelee kutawala

Elizabeth ambaye alizaliwa Aprili 21, 1926, haonyeshi dalili zozote za kustaafu, achilia mbali kuachia kiti cha Malkia. Uchunguzi wa maoni wa shirika la Ipsos MORI ulionyesha wiki iliyopita ulibaini kuwa asilimia 70 ya Waingereza wanamtaka aendelee kuwa Malkia ikilinganishwa na asilimia 21 wanaodhani anapaswa kuachia kiti hicho.

Mawaziri wa kuu wa zamani John Major na Tony Blair walimmuagia sifa Malkia Elizabeth ambapo Sir John Major alikiambia kituo cha habari cha Sky News kuwa, "ikiwa unasanifu mtu wa kuwa mtawala mkuu hapa Uingereza, nadhani ungesanifu mtu anaefanana kabisaa na Elizabeth wa pili."

Mrithi wa Major Tony Blair kutoka chama cha Labour alimsifu Malikia kwa kuufanya utawala wa ufalme kuwa wa kisasa zaidi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,rtrtv

Mhariri: Gakuba Daniel