1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 60 ya mfalme wa reggae yasherehekewa safari hii nchini Ethiopia

oummilkheir1 Februari 2005

Ethiopia inaandaa burudani ya aina pekee ;mchanganyiko wa muziki na siasa,kuadhimisha miaka 60 ya mwanarege mashuhuri ulimwenguni Bob Marley aliyefariki kwa maradhi ya cancer mwezi may mwaka 1981 akiwa na umri wa miaka 36.

https://p.dw.com/p/CHha
mfalme wa reggae
mfalme wa reggae

Muimbaji huyo aliyegeuka kitambulisho cha muziki wa reggae kutokana na nyimbo zake kwa mfano "No women No cry,Afica Unite au War",angekua na miaka 60 februrary mosi.Hii ni mara ya kwanza kwa sherehe za kumkumbuka Bob Marley kufanyika nje ya Jamaica.

Wanarasta na mashabiki zaidi ya laki mbili wa Bob Marley wamewasili katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa kushiriki katika sherehe hizo za aina yake.Mamaake,Cedella Marley Booker nae pia amefunga safari toka Florida hadi Addis Ababa ,wanakokutikana tangu mapema mwezi uliopita mjane wa Bob Marley,Rita Marley,mwanawe Ziggy na jamaa wengine wa familia yake.

Kuanzia jana jumanne mji mkuu wa Ethiopia umegeuka kitovu cha sherehe za kila aina,kuanzia burudani,warsha,maonyesho na vivutio vyenginevyo wakitarajiwa kuhudhuria zaidi ya watu laki nne,wengi kati yao ni wa kutoka nje ya Ethiopia.

Ethiopia inaangaliwa na Rita Marley kua ni mji mkuu wa Afrika,mahala yanakokutikana makao makuu ya umoja wa Afrika,na ngome ya imani ya rastafari anayojitambulisha nayo Bob Marley.

"Bob Marley aliweka nadhiri ya kurejea Ethiopia na kugeuka rastafari"Amesema Rita Marley ambae hakuondowa uwezekano wa mwili wa Bob Marley kuondolewa Jamaica na kuzikwa Ethiopia.

"Ilikua ndoto yake na ndoto ya familia yetu kumzika Ethiopia amesema bibi Rita Marley wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari .Hakutaja lakini lini wanapanga kuuhamishia Ethiopia mwili wa mfalme huyo wa Reggae.

Maadhimisho ya miaka 60 tangu Bob Markey alipozaliwa-yaliyopewa jina " Africa Unite"-kichwa cha maneno cha nyimbo mojawapo mashuhuri ya Bob Marley yamelengwa miongoni mwa mengineyo kukusanya fedha kwaajili ya miradi ya kuwasaidia wasiojiweza na waliofikwa na maafa-ikiwa ni pamoja na wahanga wa gharika ya Tsunami nchini Somalia.

Ujenzi wa kituo cha vijana katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa,na kumbusho kwaajili ya mfalme wa zamani wa Ethiopia Haile Selassie anaeangaliwa kua kiongozi wa aimani ya rastafari,navyo pia vitagharimiwa kwa fedha zitakazopatikana wakati wa sherehe hizo zilizofunguliwa jana mjini Addis Ababa kwa gwaride la vijana kwaajili ya amani na burudani ndogo iliyoongozwa na mamaake Bob Marley,Cedella Marley Booker mwenye umri wa miaka 80.

Burudani ya waimbaji wa kike itafanyika ijumaa ijayo,wakishiriki waimbaji wa kundi la Bob Markley 1-Three,na mwanamuziki wa kutoka Benin Angélique Kidjo.

Maonyesho ya sanaa ya bara la Afrika na mikutano mitatu kuhusu umoja wa bara la Afrika,wakinamama na vijana itafanyika kuanzia leo hadi ijumaa,mada ambazo ni kitambulisho cha nyimbo tatu za Bob Marley:Africa Unite,No Woman No Cry na Redemption Song.

Ijumamosi ijayo sanamu la Bob Marley litawekwa katika njia panda ya mjini Addis Ababa na Rita Marley anatazamiwa kutoa kitabu chake alichokipa jina "Maisha yangu pamoja na Bob Marley.

Jumapili february sita usiku ndio kilele cha maadhimisho ,burudani kubwa kabisa itakapofanyika katika uwanja uliojengwa upya kwaajili hii wa Meskel Square mjini Addis Ababa.Burudani hiyo itawaleta pamoja familia ya Bob Marley waimbaji wa kutoka Senegal Babaa Maal na Youssou Ndour,Angelique Kidjo,Teddy Afro wa Ethiopia pamoja na Shaggy na India Arie na wanamuziki wengine kadhaa wa bara la Afrika.

Hatimae february 11 hadi 13,burudani kadhaa zinatazamiwa kufanyika Shashemene mji ulioko umbali wa kilomita 230 kusini mwa addis Ababa wanakoishi watu wa jamii ya rastafari tangu mwaka 1948.Binafsi Bob Marley aliwahi kuutembelea mji huo alipofika ziarani nchini Ethiopia miaka miwili kabla ya kufariki dunia.

Fedha jumla za sherehe hizi zinazogharimiwa kwa pamoja na serikali ya Ethiopia,shirika la UNICEF,Umoja wa Afrika,benki kuu ya dunia na kamisheni ya kiuchumi ya umoja wa Afrika zinatajikana kufikia dala milioni moja.

.