Miaka 50 tangu Obote alipoipindua katiba Uganda
14 Aprili 2016Awe rais wa maisha Yoweri Museveni au Idi Amin kabla yake, historia ya Uganda imeghubikwa na watu walioingia madarakani kwa msaada wa kijeshi.
Wanasiasa wa upinzani kama vile Kizza Besigye hawachoki kukumbusha kila mara kwamba nchini Uganda hakujawahi kuwepo na ubadilishanaji madaraka wa amani tangu uhuru.
Msingi wa hili uliwekwa na kiongozi mwingine wa Uganda: Milton Obote. Miaka 50 iliyopita, tarehe 15 Aprili 1966, aliisimamisha katiba ya Uganda na kujitangaza kuwa rais.
Pia alimlazimisha kwenda uhamishoni Edward Mutesa II, Mfalme wa Buganda na rais wa Uganda wakati huo. Baganda walikuwa kabila lililopendelewa zaidi na Wakoloni wa Kiingereza.
Kwa Winston Churchill wakati huo akiwa naibu waziri anaehusika na makoloni ya Uingereza, Baganda walikuwa watu wastaarabu, alisema mtaalamu wa Historia Frank Schubert katika mahojiano ya DW. Ni ufahamu huu kwamba Baganda walikuwa watu maalumu, uliochochea harakati za Wasomi wa Kiganda kutaka madaraka.
Uendelezaji mgogoro wa muda mrefu
Milton Obote alikuwa mtu wa Kabila la Walang'o kutoka kaskazini mwa Uganda, na alikuwa akipinga madai ya Baganda kuwa na haki za kuchukuwa madaraka na pia urithi wa zama za ukoloni.
Kupitia muungano wake wa Uganda People's Congress UPC - uliokuwa na wanachama kutoka nchini kote, lifanikiwa kushinda wingi bungeni. Tofauti na Kabaka Mutesa aliekuwa na maono ya kuendeleza utamaduni wa ukoloni, wanasiasa wa wakati huo waliona fursa kwa Obote kuweka mwanzo mpya.
Fikra zake za kisiasa alizipata nchini Kenya, ambako alikuwa bega kwa bega na rais wa baadae wa taifa hilo mzee Jomo Kenyatta kuongoza mwamko mpya wa Kiafrika.
Kwa kumpeleka uhamishoni mfalme wa Buganda, Obote alijihakikishia uungwaji mkono wa raia wa Uganda kutoka eneo la kaskazini na pia waliokuwa katika maeneo mengine ya Uganda wasio na uhusiano na ufalme wa Buganda.
Urithi wa Obote: Taifa la kijeshi
Mtaalamu wa historia Frank Schubert anasema mapinduzi ya Obote yalibainisha wazi kabisa kwamba jeshi ni taasisi muhimu katika utatuzi wa matatizo ya ndani ya kisiasa, na kwamba viongozi wa kisiasa kama Obote wasingeona haya kulitumia jeshi, hata kwa kulibebesha jukumu kubwa la kujiimarisha.
Historia imeenea mapinduzi ambayo hayakupelekea kuwepo na serikali za kiraia. Mwaka 1971 Obote alipinduliwa na Idi Amin na akaenda kujichimbia uhamishoni nchini Tanzania, ambako alipambania na hatimaye kurudi madarakani mwaka 1980 - kabla ya kuondolewa tena miaka sita baadae na rais wa sasa Yoweri Museveni.
Museveni mwenyewe ambaye alitokea kwenye tawi la vijana la chama cha Obote cha UPC, ametumia njia mbalimbali kuzigawa jamii ambazo Obote alizihodhi kabla yake.
Kupitia jeshi lake la waasi ambao kwa sehemu kubwa walikuwa wanatokea Magharibi mwa Uganda, alifanikiwa kulishinda jeshi la serikali lililokuwa linadhibitiwa kwa sehemu kubwa na maafisa kutoka kaskazini hasa Walango na Wacholi.
Mbinu za Museveni
Tangu mwaka 1986 Museveni alifanikiwa kujenga mfumo ambao unamhakikishia kukaa madarakani mwa miongo kadhaa. Lakini mbinu zake zinafanana sana na za Obote kwa njia kadhaa.
Katika mapambano dhidi ya kundi la waasi wa LRA kaskazini mwa Uganda, Museveni anarudia ulinganifu kati ya makundi ya wakaazi mbalimbali, na anaongeza bajeti ya jeshi kila mara.
Na kama ilivyokuwa kwa Obote, anawaacha huru wanajeshi wake, hata wakati baadhi yao wametuhumiwa kwa kufanya unyama kaskazini mwa nchi.
Mwandishi: Philipp Sandner
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Grace Patricia Kabogo