1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 tangu kuuawa J. F. Kennedy

22 Novemba 2013

Marekani leo inaadhimisha miaka 50 tangu kuuawa kwa kupigwa rais wa 35 wa nchi hiyo, John F. Kennedy, mjini Dallas tarehe 22 Novemba mwaka 1963 akiwa na umri wa miaka 46, na hivyo kuuzima mshumaa wa matumaini kwa wengi.

https://p.dw.com/p/1AMKv
Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy
Rais wa zamani wa Marekani, John F. KennedyPicha: Getty Images/Keystone/Hulton Archive

''Ich bin ein Berliner,''hayo ni maneno aliyoyazungumza aliyekuwa rais wa Marekani, John F. Kennedy, wakati wa hotuba yake aliyoitoa mjini Berlin, Ujerumani wakati nchi hiyo ilipokuwa imegawanyika sehemu mbili, ya Mashariki na Magharibi.

Hii leo ikiwa inakumbukwa miaka 50 tangu kuuawa kwake, matukio kadhaa yatafanyika ikiwemo kugonga kengele za Kanisani, kuweka mashada ya maua kwenye kaburi lake, watoto kuimba nyimbo, bendera zitapepea nusu mlingoti na kusoma hotuba zilizowahi kutolewa na Kennedy.

Wakazi wa Dallas kukusanyika Dealey Plaza

Maelfu ya wakaazi wa Dallas watakusanyika kwenye eneo la Dealey Plaza, ambako msafara wa Rais Kennedy ulipita wakati alipopigwa risasi na kuuawa majira ya sita na nusu (12:30) mchana.

Rais Obama na mkewe Michele, wakiweka shada la maua kuadhimisha miaka 50 tangu kuuawa Kennedy
Rais Obama na mkewe Michele, wakiweka shada la maua kuadhimisha miaka 50 tangu kuuawa KennedyPicha: picture-alliance/dpa

Akitoa amri ya bendera kupepea nusu mlingoti hapo jana Alhamisi, Rais Barack Obama aliuelezea utawala wa Kennedy uliokuwepo wakati wa utawala wa mzozo wa makombora ya Cuba, wakati wa Vita Baridi na katika juhudi za kutetea haki za Wamarekani weusi na wanawake wa Marekani. Rais Obama amesema urithi wake hauna budi kukumbukwa siku zote.

Sauti ya Kennedy inaendelea kuwepo katika historia ya Wamarekani wengi na hasa katika hotuba yake aliyoitoa siku alipoapishwa kuwa rais wa Marekani Januari 20 mwaka 1961, aliposema, nanukuu ''Msiulize nchi yenu itawafanyia nini, Uliza wewe utaifanyia nini nchi yako?'', mwisho wa kunukuu.

Siku ya Jumatano Rais Obama alipongeza juhudi zote zilizofanywa na Kennedy, wakati akitoa nishani maalumu za uhuru za Rais.

Obama kukutana na wajumbe kadhaa Ikulu

Aidha, katika kuadhimisha siku hii mjini Washington, Rais Obama atakutana faragha na viongozi na wajumbe wa kujitolea wa kutoka kwenye mpango wa watetezi wa amani ulioanzishwa kwa kumuenzi Kennedy, kwenye Ikulu ya Marekani.

Kennedy akikimbizwa hospitali baada ya kupigwa risasi
Kennedy akikimbizwa hospitali baada ya kupigwa risasiPicha: picture-alliance/Everett Collection

Huko Boston maktaba ya John F. Kennedy itafunguliwa leo kwa ajili ya kuonyesha picha na vifaa mbalimbali vilivyotumika wakati wa mazishi ya kitaifa ya Kennedy ambazo hazijawahi kuonyeshwa hapo kabla.

Kennedy ni rais wa nne wa Marekani kuuawa akiwa madarakani, lakini mauaji yake ni ya kwanza kurekodiwa kwenye mkanda wa video.

Wengi wanakataa kuamini kuwa mauaji hayo ni njama iliyofanywa na mtu mmoja pekee mwanajeshi wa kikosi cha majini, Lee Harvey Oswald, aliyekuwa na umri wa miaka 26 wakati huo, aliyeelekeza bunduki nje ya dirisha moja kwenye chumba kilichokuwa ghorofa ya sita na kuufyatulia risasi msafara wa rais.

Lee Harvey Oswald, aliyemuuwa Kennedy
Picha ya Lee Harvey Oswald, aliyemuuwa KennedyPicha: Reuters

Shule, maeneo ya makumbusho, maktaba na makanisa kuzunguka Marekani, pia yataadhimisha kumbukumbu hiyo, kwa kuonyesha mambo mbalimbali pamoja na kutoa mihadhara. Kennedy atakumbukwa kwa kuwahamasisha watu kushiriki katika harakati za kijami na watu wengi nchini Marekani bado wanao moyo huo. Nchini Ujerumani kumbukumbu hiyo pia inaadhimishwa mjini Berlin.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE, APE
Mhariri:Yusuf Saumu