1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 tangu Dalai Lama kuikimbia Tibet

M.Bölinger - (P.Martin)10 Machi 2009

Leo inatimia miaka 50 tangu kiongozi wa kidini wa Watibet Dalai Lama kuondoka Lhasa na kukimbilia Dharamsala nchini India.Kabla ya hapo,ilionekana kana kwamba serikali ya Tibet ilielewana na watawala wa Kichina.

https://p.dw.com/p/H8k6
At the first National People's Congress in Beijing, China, on October 13, 1954, the Tibetan spiritual leader, the 14th Dalai Lama, left, shakes hands with Mao Tse-Tung; shortly after Mao's selection as chairman of the People's Republic of China. The Dalai Lama was quoted by Beijing radio as thanking the Communist leaders of China for reconstruction work in Tibet, which was invaded and occupied by Communist Chinese troops in 1950. (AP Photo)
Dalai Lama (kushoto)alipokutana na Mao Tse-Tung katika Bunge la Taifa mjini Beijing,Oktoba 13,1954.Picha: AP

Vikosi vya China vilipovuka mpaka wa Tibet hapo mwaka 1950 vilikumbana na upinzani mdogo tu.Jeshi dogo la Tibet wala halikumiliki silaha za kisasa kuweza kukabiliana na jeshi la ukombozi wa umma. Miezi michache baadae ujumbe wa Dalai Lama mjini Peking ulishinikizwa kutia saini makubaliano kuwa Tibet ni sehemu ya China.Badala yake mkataba huo wenye vipengele 17 umewahakikishia Watibet uhuru wa kujiamulia masuala ya ndani na kwamba mfumo wa kisiasa hautoguswa.Dalai Lama alikwenda Peking mwaka 1954 na alipokewa na viongozi wa serikali na umma uliomshangilia. Akateuliwa kuwa Makamu-Mwenyekiti katika bunge la taifa na akatoa hotuba kueleza mpango wa kuundwa serikali ya Tibet.Alisema:

"Maendeleo ya kila mkaazi yatazingatiwa katika katiba na sheria za utawala wa ndani ili tunufaike kutokana na haki ya kujitawala wenyewe."

Dalai Lama alikutana na Mao Tse Tung mara nyingi na alivutiwa nae sana. Katika kitabu cha maisha yake,Dalai Lama ameeleza jinsi alivyotazamia uwezekano wa Tibet kuungana na Jamhuri ya Watu wa China.Alivutiwa na mfumo wa ujamaa.Lakini aliporejea nyumbani, Dalai Lama alianza kuwa na mashaka kuhusu vitendo vya China.Mara kwa mara akagundua kuwa makubaliano yaliyopatikana, hayakuheshimiwa na majeshi ya China.Kinyume na vile ilivyoahidiwa, China iliingilia kati masuala ya kisiasa huko Tibet.Hata dini yao ilizidi kuingiliwa na Wakomunisti.Umma wa Tibet ulizidi kuhamakishwa na watawala wapya.

Mwezi Machi mwaka 1959 Dalai Lama alialikwa makao makuu ya China lakini aliambiwa kwenda peke yake.Mara uvumi ukaenea katika mji mkuu wa Tibet Lhasa kuwa Wachina wamepanga kumteka nyara Dalai Lama. Tarehe 10 mwezi Machi umati uliotaka kumlinda ulikusanyika nje ya kasri lake.China ikaambiwa iondoke Tibet.Hali ya mvutano ilipozidi baada ya machafuko kuzuka,viongozi wa ngazi ya juu na familia ya Dalai Lama walitoroshwa na baadae Dalai Lama alievishwa koti la kijeshi aliwafuata wenzake.Siku chache baadae wanajeshi wa China walianza kulishambulia kasri la Dalai Lama.Lakini wakati huo yeye alikuwa njiani kukimbilia India.Wakimbizi wa Tibet waliruhusiwa na India kuishi katika mji wa milimani Dharamsala. Suala la Tibet linaendelea kuzusha mabishano katika jumuiya ya kimataifa.