1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 40 tangu Guinea ya Equator kuwa huru

Miraji Othman14 Oktoba 2008

Miaka 40 ya uhuru wa Guinea ya Eqautor

https://p.dw.com/p/FYww
Barabara katika mji mkuu wa Guinea ya Equator, MalaboPicha: Renate Krieger

Ikiwa karibu imefunikwa na Nigeria na pia Gabon, nchi ya Guinea ya Equator karibu haionekani katika ramani. Lakini tangu kugunduliwa mafuta, hamu ya watu kujuwa zaidi juu ya nchi hiyo ndogo imeongezeka. Jumapili iliopita nchi hiyo ilitimiza miaka 40 tangu kuwa huru kutoka utawala wa kikoloni wa Kihispania. Punde baada ya uhuru, ilifuata miaka kumi na moja ya utawala wa mabavu uliosababisha kumwagika damu nyingi, chini ya Rais Francisco Macias Nguema. Lakini kuendewa kinyume haki za binadamu katika nchi hiyo ndogo ilioko katika Ghuba la Guinea hakutiliwi maanani na nchi nyingi za Magharibi. Guinea ya Equator ilikuwa moja wapo ya nchi maskini sana katika bara la Afrika, ni kama kidoto kilichosahauliwa katika mwambao wa Afrika Magharibi. Lakini mambo yalibadilika mwaka 1996, pale mafuta yalipogunduliwa. Hivi sasa nchi hiyo inatoa mapipa laki nne ya mafuta kila siku, hivyo kuwa mtoaji mkubwa watatu wa mafuta barani Afrika chini ya Jangwa la Sahara. Lakini licha ya utajiri huo, nchi hiyo imejionea maendeleo machache sana, kiuchumi na kisiasa, Na licha ya kwamba wawekezaji wa kigeni wana hamu ya kujishughulisha katika nchi hiyo, lakini maendeleo hayajawafikia watu wa kawaida.

Katika kutafuta visima vipya vya mafuta, tena katika mazingira ya usalama, nje ya Mashariki ya Kati, mwanzoni mwa karne hii, Marekani ililikodolea macho eneo la Ghuba ya Guinea. Karibu ya thuluthi moja ya hifadhi ya mafuta ya Afrika yako chini ya bahari ya mwambao wa Afrika Magharibi na Kati. Wamarekani wamegundua mafuta yalio myepesi na yalio bora kabisa.

Katikati ya mji mkuu wa Malabo, ambao uko katika kisiwa cha Bioko, karibuni kutajengwa bandari ya kisasa. Na kama vile katika maeneo mengi ya Guinea ya Equator, mtu anajionea ujenzi mkubwa wa miundo mbinu.

Hilo ni karandinga linalokwenda huko na kule, ili kuiweka sawa barabara. Na katika jukwaa kuna makrini mawili yakibeba michanga na kuimwaga majini. Upande wa kushoto wa ukingo wa bahari, kuna meli ambayo inapakiwa shehena za mizogo.

Günter Tröster, mfanya biashara wa Kijerumani, punde hivi amewasili Guinea ya Equator, na baada ya siku mbili tu ameshazigundua nafasi kwa biashara ya kampuni yake ya Mero TSK inayoshughulika ujenzi wa mapaa na kuuza vifaa vya ujenzi.

" Kwanza ni suala la mawasiliano. Kuna ndege ya moja kwa moja, kwani kwa wafanya kazi hilo ni jambo muhimu kwa vile inagharimu fedha nyingi ikiwa wasafiri kutoka kona tatu za dunia wakisubiri usafiri kila mahala. Kutoka Angola iliwabidi wasafiri kupitia Lisbon, na kuwa safarini hadi wanapowasili hapa, hadi wanapokuweko katika kiwanja cha ndege na kwenda hotelini. Ni janga."

Huenda akapata karandasi ya kujenga paa la kiwanja cha ndege kipya ambacho kinajengwa katika sehemu ya bara ya Guinea ya Equator, ambayo licha ya kisiwa cha Bioko kilicho na mji mkuu wa Malabo, ni kipande cha ardhi cha kona nne baina ya Kamerun na Gabon. Bwana Tröster anaziona faida za kuwekeza katika Guinea ya Eqautor.

" Kwa hivi sasa nchi hii ni tulivu, rais wake amekuwa madarakani kwa muda mrefu. Angalau sasa mtu anaweza kutabiri hali ya mambo, lakini ikiwa kila baada ya miezi anakuja kiongozi mpya, mambo yatakuwa hayatabiriki. Hata kama mambo yanaonekana kuwa magumu, lakini ni bora kuliko kwetu huko Ujerumani ambako kila baada ya miaka minne chama kipya kinachaguliwa."

Inatambuliwa duniani kote kwamba haki za binadamu zinaendewa kinyume katika nchi hiyo, rushwa imesheheni na kuna utawala wa mkono wa chuma wa Rais Teodoro Obiang unaowakandamiza wakaazi nusu milioni wa Guinea ya Equator.

Wawekezaji wa kimataifa wanaipenda Guinea ya Equator, kwani kinyume na nchi nyingine za Afrika, serekali ya nchi hiyo haidai sehemu kubwa ya faida ya biashara. Hasa wafanya biashara wa Kimarekani wamedhibiti uchumi wa mafuta na raia wa Kimarekani hawahitaji kuwa na viza kuingia nchini humo. Wahakiki wanasema hali hiyo haijailetea nchi hiyo ya Kiafrika mikataba yenye faida, na ndio maana sasa kuna majaribio kwamba licha ya Wamarekani, pia wawekezaji wengine waalikwe kuchangia katika uchumi. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya taifa ya mafuta, Sonagaz, Juan Antonio Ndong, anasema:

" kutokuweko ushindani, na biashara kuendeshwa na mtu mmoja tu, sio fikra nzuri. Mtu anakuwa hajuwi kama anachofanya ni sawa. Tunawapenda Wamarekani, lakini lazima pia tubadilishe. Siwalaumu Wamarekani. Wajerumani, kwa mfano , kwetu sisi ni wafanya biashara wenye kuvutia. Wanabakia na kauli yao, wakweli."

Kunapangwa pia kujenga ghala nyingine ya kuhifadhiwa gesi iliobadilishwa kuwa maji maji, na wawekezaji katika mradi huo ni kampuni ya Kimarekani ya Narathan, ile ya Kihispania, Union Fenosa, na ya Kijerumani Eon. Friedrich Oschmann wa kampuni ya Kijerumani ya Eon anasema:

" Hisia zangu ni nzuri kwa nchi hii, pia kwa watu wanaobeba dhamana ya nchi hii. Mnamo miezi nimeweza kujenga mahusiano ya kibinafasi na wafanya biashara muhimu. Na muhimu zaidi inahitaji ukataji uamuzi ufanyike katika ngazi za chini, sio ungoje wakubwa wa juu. Mambo mengi hapa huamuliwa katika ngazi ya dola, na maamuzi hayatakiwi kubishwa. Bila ya kibali cha rais, mambo hayaendi."

Licha ya neema ya mafuta, Guinea ya Eqauator ina maendeleo duni; katika orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, nchi hiyo iko 127 kati ya nchi 177 linapokuja suala la maendeleo.

Matthias Stefan, kijana aliyezaliwa Marekani, lakini ni mtoto wa mmishinari wa Kijerumani, ameishi Malabo kwa miaka kumi, na ana haya ya kusema:

"Lazima uangalie huku na kule, pande zote, ikiwa kuna mtu anakuangalia au anakusikiliza unachosema. Naweza kusema hapa kuna demokrasia nusu na udikteta nusu. Hivi sasa marafiki zangu wananiambia kwamba inafaa nijichunge kidogo, nisizungumze sana, nisijichongee sana."

Mtu anaweza kuihisi hali ya kutisha katika mji wa Malabo. Hata watoto wanaocheza katika uwanja mkubwa mbele ya Kasri ya Rais huangaliwa na wanajeshi. Kamera hazionekani, na pia vinasaji sauti. Mtu anapouliza kwanini, anajibiwa kwamba kila raia wa Guinea Bissau ni mwanajeshi. Hiyo ina maana kila mkaazi wa nchi hiyo anajaribu kuilinda nchi yake, hasa dhidi ya raia wa kigeni.

Hofu hiyo ya kupindukia mipaka imeongezeka tangu mwaka 2004, wakati lilipofanywa jaribio la mapinduzi la askari 70 wa kukodiwa na kushindwa. Raia wa Kiengereza, Simon Mann, aliyekuwa kiongozi wa jaribio hilo tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ametiwa gerezani huko Malabo.

Na licha ya ya utawala wa karibu miaka thalathini wa Teodore Obiang, yaonesha demokrasia bado ingalia ikingojewa huko Guinea ya Eqauator. Bungeni, viti 99 kati ya 100 ni vya mseto wa vyama ambavyo vinaungwa mkono na Rais Obiang. Upande wa upinzani una mbunge mmoja tu. Na katika uchaguzi wa urais hapo mwakani, Obiang inatazamiwa sana atachaguliwa tena.