1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 32 ya uhuru wa Zimbabwe

18 Aprili 2012

Zimbabwe inasherehekea miaka 32 tangu kupata uhuru kutoka kwa watawala wa kikoloni. Lakini licha ya kuwa huru kwa muda mrefu, Zimbabwe inayoongozwa na Rais Robert Mugabe, bado inakumbwa na matizo mengi.

https://p.dw.com/p/14fdi
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: Reuters

Chipukizi wa chama tawala, jeshi la vijana, wapiganaji wa zamani pamoja na wafuasi wa chama tawala kutoka pande zote za Zimbabwe leo watasherehekea uhuru wa nchi yao. Tarehe 18. Aprili mwaka 1980 ilikuwa siku iliyojawa na matumaini kwa watu wa Zimbabwe. "Umeshika lulu mikononi mwako na hivyo itunze." Hayo ndiyo maneno ambayo Samora Machel, aliyekuwa rais wa Msumbiji na Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania, walimwambia Robert Mugabe siku ambapo Zimbabwe ilipata uhuru.

Leo, miaka 32 baadaye, nchi hiyo imegubikwa na umaskini. Utawala uliopo sasa haufanyi tena kazi ipasavyo. Andreas Sibanda ni mkimbizi kutoka Zimbabwe. Yeye anamlaumu rais Mugabe kwa kushindwa kuipatia nchi yake uhuru wa kweli. Kwa mtazamo wake, raia wa Zimbabwe sasa wanateseka zaidi kuliko hata ilivyokuwa wakati wa utawala wa kikoloni.

Raia wengi wa Zimbabwe wanaishi katika hali ya umaskini
Raia wengi wa Zimbabwe wanaishi katika hali ya umaskiniPicha: AP

Washington Chiula, ambaye pia ni raia wa Zimbabwe, anaupinga utawala wa Mugabe. Anajiuliza inakuwaje Zimbabwe inajiona kuwa nchi huru wakati asilimia 90 ya raia hawana ajira, wapinzani wa kisiasa wanagandamizwa na watu wanakamtwa na polisi bila hatia. "Kila siku wapo watu wanaokamatwa bila kuwa na hatia. Hakuna demokrasia. Hatuwezi kusema kwamba tuko huru wakati hakuna demokrasia."

Wazimbabwe wengi wanaishi uhamishoni

Chiula anaeleza kwamba asilimia 30 ya raia wa Zimbabwe, ambao ni watu wapatao millioni 5, wamefukuzwa kutoka nchini mwao katika miaka 11 iliyopita. Mmoja wao ni Noel Mguti. Yeye alitekwa nyara na kuteswa. Nyumba yake ilichomwa moto na kuteketea kabisa. Mke wake alipotea na hadi leo haifahamiki mahali alipo.

Wakimbizi wakitafuta hifadhi katika ubalozi wa Afrika Kusini
Wakimbizi wakitafuta hifadhi katika ubalozi wa Afrika KusiniPicha: picture-alliance/ dpa

Kwa sasa Mguti anaishi uhamishoni Afrika ya Kusini akiwa na msononeko mkubwa. "Nitawezaje kusherehekea uhuru wakati akili yangu haiko huru?" Anauliza Mguti. "Wala siko huru katika nchi niliyokimbilia. Kwa kweli Zimbabwe haikuwa na uhuru. Watu waligandamizwa na rais wao mwenyewe. Mugabe ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa sababu hakuwapatia Wazimbabwe uhuru."

Karibu kila raia wa Zimbabwe anayeishi uhamishoni ana mawazo kama aliyonayo Mguti. Mugabe hatazamwi tena kama kiongozi aliyeiletea nchi yake uhuru bali kama mtawala anayewafanya raia wake wateseke.

Mwandishi: Claus Stäcker

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman