Miaka 100 ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia
3 Agosti 2014Viongozi hao wawili wamekutana huko Hartmannswilerkopf kuwakumbuka wanajeshi 30,000 walipoteza maisha yao katika mapigano makali ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia kwenye eneo la kilele cha mlima wa majabali katika mkoa wa Alsace karibu na mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Hollande ametowa hotuba nzito kwa kuwataka wahusika wa mzozo wa Gaza kuweka kando uhasama wao kama vile walivyofanya Ufaransa na Ujerumani.Amesema Ufaransa na Ujerumani ambazo zilikuwa zikihesabiwa kuwa na uadui wa urithi zimeweza kupatana na ameitaka dunia itumie amani ilioko kati ya Ujerumani na Ufaransa kama funzo katika juhudi za kuleta amani na kuzuwiya mateso ya raia huko Gaza.
Katika hotuba zao Hollande na Gauck sio tu wamekumbuka muhanga uliotolewa bali pia wamegusia urafiki wa nchi zao na ujenzi wa bara la Ulaya lenye amani baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Pili vya Dunia. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa taifa la Ujerumani kuhuhudhuria tukio hilo.
Matukio ya kumbukumbu
Mwaka jana viongozi hao wawili walifuatana bega kwa bega kuelekea kwenye eneo la kumbukumbu kati kati ya kijiji cha Ufaransa cha Orador-sur- Glane ambapo vikosi vya Ujerumani vya SS viliwauwa watu 642 hapo Juni 10 mwaka 1944 wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia huo ukiwa ni unyama mkubwa kabisa kufanywa na Wanazi kwa Ufaransa iliokuwa ikiikalia kwa mabavu.Gauck pia alikuwa ni kiongozi wa kwanza kabisa wa Ujerumani kuwahi kukitembelea kijiji hicho.
Huko Hartmannswillerkopf, Hollande na Gauck wameweka mashada ya mauwa, wamebaki kimya kwa dakika moja na kukutana na wanafunzi wa Ujerumani na Ufaransa takribana 100 wanaoshiriki katika mpango wa kubadilishana wanafunzi kati ya nchi hizo mbili.
Pia wameweka jiwe la msingi kwa ajili ya makumbusho ya kwanza iliobuniwa na wanahistoria kutoka nchi hizo mbili ambayo itakuwa ina simulizi za mapigano katika mlima unaojulikana kwa Kifaransa kama "Vieil Armand" yaani "Mlima Wenye Kula Watu"
Urafiki una nguvu
Ofisi ya Hollande imesema matukio hayo ni ushahidi wa nguvu ya urafiki uliopo kati ya nchi hizo mbili ambao unawawezesha kutafakari kwa pamoja historia yao ya pamoja kikiwemo kile kilichokuwa kibaya kabisa.
Ofisi hiyo ya rais imeongeza kusema kwamba "Ishara hiyo ina nguvu zaidi kotokana na kwamba tarehe tatu Augusti mwaka 1914 ilianzisha kipindi cha miaka 30 ya mizozo, machungu,mauaji ya watu wengi na unyama kati ya Ufaransa na Ujerumani."
Wakati huo huo vizazi vya waathirika wa kwanza wa vita hivyo hapo Jumamosi walikusanyika katika mji wa Ufaransa wa mpakani ulioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wa Joncherey kwa ajili ya kumbukumbu ya karne moja ya mauaji yao ambayo yalitokea katika mkesha wa tangazo la vita la Ujerumani dhidi ya Ufaransa wakati vikosi vya Ujerumani vikiwa katika shughuli za upelelezi vilipowashambulia kwa risasi wanajeshi wa Ufaransa.
Athari ya Vita Vikuu
Mzozo huo wa miaka minne ambao ulikuja kujulikana kama Vita Vikuu uliuwa zaidi ya watu milioni 12 na milioni nne kati yao wakiwa raia na kuwajeruhi wengine milioni 20 katika medani za mapambano. Mamilioni wengine walipoteza maisha yao kutokana na kukaliwa kwa mabavu,magonjwa, njaa au kurudishwa kwenye nchi za asili zao kwa nguvu.
Vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vimeacha alama isiofutika kwa Ufaransa na Ujerumani na matukio yaliopelekea kutangazwa kwa mzozo huo wa miaka minne yalianzia na kuuwawa kwa Archduke Franz Ferdinand mrithi wa himaya ya kifalme ya Austria na Hungary hapo Juni 28 mwaka 1914.
Katika kipindi cha miaka 37 iliofuatia,tawala za himaya za Ulaya zilijikuta zikitumbikia kwenye mzozo wa kidiplomasia uliosababishwa na miungano iliokuwa migumu na kulazimika kuchaguwa upande wa kuunga mkono kwa vita vilivyofuatia.
Uharibifu wa kisiasa ulioachwa na Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia ulikuja kuwa mbolea iliochochea kusimama kwa utawala wa Manazi nchini Ujerumani katika miongo iliofuatia na pia kuchochea kusimama kwa Ukomunisti na kuanguka kwa Ukoloni katika karne ya 20.
Hapo Jumatatu katika mji wa Liege nchini Ubelgiji kubumbukumbu ya miaka 100 tokea Ujerumani ilipoivamia Ubelgiji itahudhuriwa na ukoo wa kifalme wa Ubelgiji na Uingereza halikadhalika wakuu wa nchi na serikali akiwemo Hollande na Gauck.
Uingereza pia itakuwa na matukio ya kumbukumbu ya miaka 100 tokea nchi hiyo ilipotangaza vita dhidi ya Ujerumani.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/DW
Mhariri : Amina Abubakar