Mhubiri wa Iraqi azishtumu Marekani na Iran.
10 Januari 2020Ayatollah Ali al-Sistani amesema kuwa mashambulizi ya pande zote mbili nchini Iraq mwezi huu yanaonyesha wazi kutojali uhuru wa Iraq na watu wake wako katika hatari ya kuathirika zaidi kutokana na mzozo huo wa Marekani na Iran. Pia hii leo, mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya walikusanyika mjini Brussels kutafuta njia za kutuliza hali tete ambayo imezuka kuanzia wiki iliyopita.
Mjini Washington, bunge limepiga kura hapo jana kuzuia hatua zaidi za kijeshi za rais Donald Trump dhidi ya Iran.
Lakini eneo hilo bado liko katika hali ya wasiwasi huku makamanda wa kijeshi wa Iran wakitishia mashambulizi zaidi na kuongeza wasiwasi kwamba hatua ya kuzuia mashambulizi huenda ikawa ya muda mfupi.
Katika taarifa iliyowasilishwa kupitia msemaji mmoja wakati wa swala ya Ijumaa katika mji mtakatifu wa Kerbala, Ayatollah Sistani amesema kuwa misururu ya mashambulizi hayo ni ukiukaji wa uhuru wa nchi hiyo na kwamba hakuna mataifa ya nje yanayopaswa kuamua hatma ya Iraq. Tangu kuuawa kwa Soleimani, Iran imeimarisha wito wake wa vikosi vya kijeshi vya Marekani kuondoka Iraqi ambayo kama Iran ni taifa lenye idadi kubwa ya wafuasi wa madhehebu ya shia.
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran hayatoshi na kwamba kile kilicho na umuhimu kwasasa ni kufikisha mwisho uwepo wa jeshi la Marekani katika eneo hilo. Wachambuzi wanasema kuwa lengo kwa sasa huenda likawa kuweka shinikizo zaidi kwa serikali ya Iraqi inayoongozwa na washia kuendelea kushinikiza kuondoka kwa Marekani na kushinikiza wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq kuvisumbua vikosi vya jeshi la Marekani.
Wakati huo huo, Ndege zisizojulikana zimelenga maeneo nchini Syria katika mpaka na Iraq hii leo na kuwauwa wanamgambo wanane wa Iraqi wanaoungwa mkono na Iran, wanaharakati wawili wa Syria na maafisa wawili wakuu wa Iraqi, shambulizi linalojiri huku taharuki ikitanda kati ya Marekani na Iran.Shirika la kufuatilia haki za binadamu nchini Syria, limesema kuwa ndege hizo zililenga maeneo yanayomilikiwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran katika eneo la Boukamal karibu na mpaka na Iraqi.
Afisa mmoja mkuu wa usalama wa Iraqi pamoja na afisa mwengine kutoka wanamgambo wa Iraqi wanaoungwa mkono na Iran wanaojulikana kama Popular Mobilization Forces , wamesema kuwa ndege hizo za kivita zililenga magari mawili yaliokuwa yamebeba makombora katika upande wa mpaka wa Syria. Wanasema kuwa shambulio hilo huenda lilitekelezwa na ndege za kivita za Israel lakini hawakutoa ushahidi wowote.